Benki ya Wanawake Tanzania yasema hali yake kifedha, kiutendaji ni imara

Muktasari:
Hayo yamo katika taarifa yake ya kukanusha habari zilizochapishwa katika gazeti hili toleo la Mei 4 zikieleza kuwa benki hiyo ni miongoni mwa zilizo hatarini kufungwa.
Dar es Salaam. Uongozi wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) umesema taasisi hiyo inaendelea kutoa huduma za kibenki kama kawaida, ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa wananchi, hasa wanawake, kwa gharama nafuu.
Hayo yamo katika taarifa yake ya kukanusha habari zilizochapishwa katika gazeti hili toleo la Mei 4 zikieleza kuwa benki hiyo ni miongoni mwa zilizo hatarini kufungwa.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TWB, George Msambazi inasema: “Benki inaendelea kuboresha huduma na kupanua matawi mpaka vijijini ili kuhakikisha mwananchi wa kawaida, hasa mwanamke, anapata huduma za kifedha kwa haraka na uhakika zaidi.”
Kauli ya TWB imekana kuwa katika hali ya kufungwa.
“Ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pekee yenye mamlaka ya kutoa tamko juu ya hatari inayoweza kusababisha benki yoyote ile kufungwa,” inasema taarifa hiyo
Habari inayolalamikiwa ilikuwa sehemu ya uchambuzi wa hali ya benki na taasisi za kifedha nchini zinazokabiliwa na hali mbaya kutokana na baadhi ya wakopaji kuonyesha kushindwa kulipa mikopo.
Mhariri anaomba radhi kwa benki, wateja wake na umma kwa jumla kwa maneno machache katika taarifa hiyo, yaliyosababisha kutoeleweka kama ilivyokusudiwa.
Habari zaidi Uk. 7