Bilioni 9 kusomesha wataalamu bingwa, bobezi

Muktasari:

  • Mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa ufadhili wa masomo na hivyo kuongeza wataalamu bingwa na bobezi sekta ya afya (Samia Health Super Specialization Program), umetoa kiasi cha Sh9 bilioni kwa ajili ya kusomesha wataalamu hao ili kukabiliana na changamoto na upungufu wa wataalamu.

Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema imepokea Sh9 bilioni kwa ajili ya mafunzo ya wataalamu bingwa na bobezi katika fani mbalimbali za sekta ya afya, na kwamba udahili wa masomo ya shahada ya uzamili umefunguliwa rasmi.

Ufadhili huo unawahusu wataalamu wa afya ambao wapo tayari katika vituo vya afya wakiendelea kutoa huduma na ambao pia ni watumishi wa afya.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Agosti 25, 2023 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, ambaye amesema lengo la mpango huo ni kuboresha na kusogeza huduma za kibingwa na bobezi, na hivyo kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi.

"Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara imetengewa jumla ya Sh9 bilioni kwa ajili ya mafunzo ya wataalamu bingwa na bobezi katika fani mbalimbali za sekta ya afya, na katika hii tunalenga yale maeneo ambayo wataalamu ni wachache, tunaongeza mabingwa na wabobezi ili kuondoa ombwe lililopo," amesema Dk Mollel.

Amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitenga kiasi cha Sh8 bilioni katika mpango huo wa masomo na mwaka huu Serikali imeongeza Sh1 bilioni.

Ametaja miongoni mwa masharti yaliyotolewa kwa waombaji, ni pamoja na kuwa kuwa Raia wa Tanzania, mtumishi wa umma na ambaye amefanya kazi kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.

Masharti mengine ni kuwa mwombaji awe anatakiwa kuthibitishwa na mwajiri wake, barua ya udahili kwenye chuo kinachotambulika, na awe anaenda kusoma masomo ya uzamili na kwamba ufadhili utazingatia maeneo yenye uhaba wa wataalamu au fani kwenye kituo husika pamoja na nyaraka mbalimbali muhimu ambazo zimetajwa katika fomu ya maombi.

Ametaja maeneo yenye wataalamu wachache nchini kuwa ni pamoja na wataalamu bingwa wa upasuaji wa mishipa na mfumo wa fahamu, ubongo, magonjwa ya moyo na fani ambazo ni za kipaumbele katika utoaji wa huduma za kibingwa.