Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Biteko ataka NGOs kuhusika uboreshaji sekta ya ardhi Afrika

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, Doto Biteko akifungua kongamano la ardhi

Muktasari:

  • Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko amezitaka taasisi za ardhi Afrika, kusaidia upatikanaji rasilimali fedha ili kutatua migogoro ya ardhi na upatikanaji hatimiliki.

Arusha. Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko amezitaka taasisi za ardhi Afrika, kusaidia upatikanaji rasilimali fedha ili kutatua migogoro ya ardhi na upatikanaji hatimiliki.

Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati, ameyasema hayo leo Jumanne, Septemba 12, 2023 jijini hapa, wakati akifungua kongamano la nne la taasisi za ardhi Afrika.

“Fanyeni tathimini ya utekelezaji maazimio ya makongamano yaliyopita, ili isaidie kuwa mkakati utakaoboresha sekta ya ardhi barani Afrika,” amesema Dk Biteko na kuongeza;

“Miaka ijayo, tajiri mkubwa duniani atakuwa ni yule ambaye anamiliki ardhi kubwa, hivyo natoa wito wito kwa wananchi kuhakikisha wanamiliki ardhi kisheria na kupata hati miliki.

Kwa upande mwingine, taasisi ya kimataifa inayoshughukia haki za umiliki wa rasilimali (RRG) barani Afrika, imeshauri serikali kusaidia jamii za pembezoni kupata haki za umiliki wa ardhi.

Rais wa taasisi hiyo Dk Solange Badji, amesema jamii ya za pembezoni barani Afrika zinakabiliwa na changamoto ya umiliki wa ardhi ya Jamii.

Amesema Jamii hiyo licha ya kuishi katika ardhi kidogo lakini hawana hati miliki ya maeneo yao na hivyo kukosa Haki za umiliki kisheria.

Amesema Jamii hizo za pembezoni na nyingine za asili zimeathirika na mabadiliko ya tabianchi.

"Changamoto za masuala ya ardhi zinafanana barani Afrika hivyo kuna haja ya kuwepo na sheria na Kanuni nzuri za umiliki wa ardhi"amesema

Hata hivyo amepongeza serikali ya Tanzania kuwa na sheria na sera nzuri za ardhi na kutaka nchi nyingine kujifunza.

Dk Badji amesema katika kusaidia jamii za pembezoni, taasisi hiyo imetoa fedha kwa  mtandao wa mashirika ya wafugaji wa asili na waokota matunda (Pingos Forums) na Ujamaa Community Resource Team (UCRT), kuwezesha kwa mradi wa ardhi kwa jamii hizo.

Mwanzilishi wa shirika la UCRT, Makko Sinandei, amesema wanatarajia kushirikiana na PINGOs Forums kusaidia upimaji wa ardhi za vijiji, utoaji elimu wa umiliki wa ardhi kwa jamii na utumiaji ardhi kiuchumi.

Mratibu wa mtandao wa mashirika wanaojihusisha na utetezi wa rasilimali ardhi (TALA), Bernard Baha amesema kongamano hilo lina umuhimu mkubwa kwani wanatarajia kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya umiliki wa ardhi barani Afrika.

Baha amesema katika kongamano hilo pia kila nchi inatarajiwa kutoa mikakati yake ya kukabiliana suala la upatikanaji hatimiliki za ardhi na kukabiliana na migogoro ya ardhi.