Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bodaboda zinavyotishia uhai wa wanafunzi

Muktasari:

Kwa mujibu wa ofisi ya takwimu ya MOI kwa mwaka 2016 walipokea watoto 1,200 wenye umri wa kati ya miaka 0-12 kutokana na ajali, robo tatu zikihusiswa na usafiri wa pikipiki.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya wanafunzi 32 wa Lucky Vincent kupoteza maisha katika ajali ya basi wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha, imebainika kuwa watoto wengi waliolazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) ni waathirika wa ajali za bodaboda.

Kwa mujibu wa ofisi ya takwimu ya MOI kwa mwaka 2016 walipokea watoto 1,200 wenye umri wa kati ya miaka 0-12 kutokana na ajali, robo tatu zikihusiswa na usafiri wa pikipiki.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa wazazi na walezi huutumia usafiri wa bodaboda kama njia mbadala ya mabasi ya shule au yale ya abiria kutokana na adha ya usafiri hapa jijini.

Wazazi huchangishana fedha na kuwapandisha watoto watatu au wanne hasa wa shule za chekechea katika bodaboda ambayo huwafikisha shuleni.

Bodaboda wanasemaje?

Dereva wa Bodaboda mwenye makazi yake maeneo ya Tegeta Ally Abdul anasema yeye ni mmoja wa wanaobeba wanafunzi kwa kutumia usafiri huo na mara nyingi hubeba wawili wawili.

“Tunapata tenda kutoka kwa wazazi, tunakubaliana malipo kulingana na umbali lakini mara nyingi bei inakuwa ndogo kwa kuwa kazi ni ya uhakika kwa kila siku na malipo yanafanyika kwa mwezi au wiki kulingana na makubaliano,” anasema Abdul.

Anasema baada ya makubalino wajibu unabakia kwake kuhakikisha mtoto anakwenda shule kila siku na kurudi na hata kama anakuwa na dharura humuomba dereva bodaboda mwenzake amsaidie kutimiza wajibu wake.

“Lakini kupakia watoto huwa nachagua kwanza wasio watundu na wale wanaopita maeneo yasiyonilazimu nipite barabara kuu. Nafanya hivyo kwa ajili ya kuepuka ajali na kukimbizana na askari,” anasema Abdul.

Dereva mwingine ambaye hufanyia shughuli zake eneo la Mwenge, Deus Tito anasema kusafirisha wanafunzi ni miongoni mwa safari ambazo humpatia fedha nyingi katika biashara yake kwa sababu ni kazi ya uhakika, kwani kila siku lazima mwanafunzi aende shule.

“Kwa sababu nakuwa katika utafutaji nafanya kazi hiyo kwa umakini. Wakati mwingine mtoto kama amechoka anaweza akajisahau akadondoka sababu ya usingizi, hata spidi nikiwa nimebeba mwanafunzi inapungua kwa sababu endapo nikimdondosha ni kesi kubwa,” anasema Tito.

Wanachosema wazazi

Mwananchi liliwahi kufanya uchunguzi kuhusu matumizi ya bodaboda kama usafiri wa kwenda shule na kuzungumza na wazazi.

Katika uchunguzi huo, mkazi mmoja wa Tabata aliyejitambulisha kwa jina la Lilian Kaiza alisema mtoto wake anayesoma Shule ya Msingi Tusime na huchukuliwa na basi la shule, lakini ikitokea kwa bahati mbaya akaachwa na basi hilo hulazimika kukodi bodaboda ili kumpeleka shule.

“Naogopa sana kutumia usafiri wa bodaboda, ila kuna siku majukumu ya kazi yangu yananitaka nitumie usafiri huo ili kuwahi shughuli ninayotakiwa kwenda kuifanya, hali hiyo imenifanya kumuamini dereva bodaboda mmoja ambaye anakaa jirani na kwangu kwasababu ni mstaarabu na yupo makini anapokuwa akiendesha,” anasema

“Kwa hiyo siku ikitokea mtoto wangu akaachwa na basi la shuleni kwao, huwa nampigia simu dereva bodaboda anaitwa Omar ili aje nyumba amchukue na akiniambia yupo mbali au yupo busy labda anitumie dereva mwingine huwa sikubali inanibidi niamke mwenye nichukue gari yangu kwa ajili ya kumpeleka mtoto shule.”

Anasema amekuwa akikutana na madereva bodaboda barabarani wakiwa wamepakiza wanafunzi zaidi ya wawili huku wakiendelea na michezo yao ya kuchomekeachomekea magari wakati wanajua wamepakiza watoto kwenye vyombo hivyo.

Mzazi mwingine, Donald Mbikinywa mkazi wa Tegeta anasema wazazi huchanga fedha kwa ajili ya usafiri wa mabasi kwa shule zinazotoa huduma hiyo ili kuondokana na usumbufu licha ya gharama za usafiri kuwa kubwa.

“Mimi nalipa Sh800,000 kwa mwaka kwa ajili ya usafiri wa watoto wangu lakini wakati mwingine gari linakuja mapema kabla hawajajitayarisha, hivyo huwa namtumia dereva bodaboda anawapeleka shuleni,” anasema Mbikinywa.

Kauli za walimu

Baadhi ya walimu wa shule za awali na msingi ambazo hazitoi huduma ya usafiri zilizopo Dar es Salaam wanasema hawajihusishi na usafiri wa wanafunzi kutoka nyumbani kwenda shuleni, bali wanajali wanafunzi wafike mapema.

Walimu walitoa kauli hiyo walipokuwa wakizungumza na gazeti hili baada ya mwandishi kuhoji juu ya wanafunzi wanaopanda bodaboda zaidi ya mmoja wanapowahi shuleni.

Walimu hao wanasema uandikishaji wa wanafunzi huzingatia umbali wa kilomita sifuri hadi tatu kutoka eneo la shule, lakini baadhi ya wazazi hukwepa kutaja sehemu halisi wanazoishi kwa hofu ya watoto wao kukosa nafasi katika shule hizo.

“Watoto wanaotakiwa kusoma shule yetu ni wale wanaoishi mazingira jirani kwa umbali usiozidi kilomita tatu ambapo mwanafuzi akiamka mapema anawahi kufika shuleni kwa miguu,” anasema mwalimu Musa Kisange kutoka Shule ya Msingi Kunduchi.

Mwalimu Mary Kitali wa Shule ya Awali ya Mtakatifu Lilian iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam anasema wazazi wenye wanafunzi zaidi ya mmoja hutumia bodaboda moja kubeba watoto wao wakati wa kwenda shule kwa kuwa kukodisha pikipiki kwa kila mwanafunzi ni gharama. “Shule yetu haina gari la wanafunzi, hivyo wanafunzi wanaoishi mbali hutafuta usafiri mbadala kufika shuleni, baadhi wanaletwa na bodaboda pamoja na bajaji. Wazazi hufanya hivi kwa makubaliano na madereva hao,” anasema Kitali.

Wanafunzi waliohojiwa na gazeti hili walisema wanalazimika kupanda bodaboda wawili au zaidi ili kupunguza gharama za usafiri huo na kila mmoja huchangia kati ya Sh100 hadi 500 kutokana na kushindwa kumudu gharama ya mtu mmoja kwa kila siku.

“Naishi Salasala hakuna usafiri wa gari tunachangia bodaboda kwa kuwa ni usafiri unaopatikana hapa kwa gharama ya Sh1,000 hadi 1,500 hatuna uwezo wa kumudu hizo gharama kwa mtu mmoja, zinasaidia kutusogeza mpaka Tegeta Kwandevu tunatembea hadi shuleni,” anasema Davis Nyamaka mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Kunduchi.

Baraka Davis ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Pius Msekwa anasema wakati wa masika kuna wakati huteleza na kuanguka katika bodabaoda kutokana na ubovu wa barabara eneo la Salasala kwa Babu jijini Dar es Salaam.

“Tukipata matatizo njiani hatusemi kwa walimu tunakausha, niliwahi kuanguka na mwenzangu nikaumia mkono hadi nilishindwa kuandika shuleni, nyumbani walinionya wakasema niwe mwangalifu,” anasema Baraka.

Usalama barabarani

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabara nchini, Kamanda Mohamed Mpinga anawataka madereva bodaboda kufuata taratibu na kanuni za usalama barabarani.

Anasema polisi itaendesha operesheni nchi nzima ili kupambana na madereva bodaboda wanaokiuka sheria za usalama barabarani ikiwamo kupakia wanafunzi kwa mtindo wa mishikaki. “Nitatoa maelekezo kwa wakuu wote wa vikosi vya usalama barabarani nchini kuzuia suala hili na watakaobanika watachukuliwa hatua za kisheria,” anasema.

Wizara inasemaje?

Katika bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba alisema ajali nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva, kutozingatia sheria za usalama barabarani, mwendokasi, ulevi pamoja na ubovu wa vyombo vya usafiri na miundombinu.