Bodi ya nafaka yatenga Sh100 bilioni kununua mazao nchini

Mwenyekiti wa CPB, Salum Awadhi (wakwanza kushoto) akizungumza kwenye kikao na wadau wa kilimo kilichofanyika jijini Mwanza. Wa pili kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CPB, John Maige. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko nchini (CPB) imetenga Sh100 bilioni kununua tani 115, 000 ya mazao nchi nzima kwa mwaka wa fedha 2023/24 unaoanza Julai mwaka huu.

Mwanza. Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko nchini (CPB) imetenga Sh100 bilioni kununua tani 115, 000 ya mazao nchi nzima kwa mwaka wa fedha 2023/24 unaoanza Julai mwaka huu.

Akizungumza Mei 20, 2023 kwenye kikao cha wadau wa kilimo Kanda ya Ziwa kilichofanyika jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi CPB, Salum Awadhi amesema kiwango hicho kimetengwa ili kumuwezesha mkulima kuwa na soko la uhakika litakalosaidia kuongeza chachu ya uzalishaji.

“Mwaka huu wa fedha unaoanza Julai tumejiwekea bajeti ya bilioni 100 kununua mazao nchi nzima kutokana na mahitaji yetu na viwanda tulivyonavyo,” amesema

Amewataka wakulima na wafanyabiashara kutumia miundombinu ya bodi hiyo kuhifadhia mazao yao akidai asilimia 40 ya mazao yanayovunwa nchini uharibika kutokana na kushindwa kuhifadhiwa vizuri.

“Sisi tunataka tujenge viwanda ili watu walete mazao yao sisi tuyachakate, tuongeze thamani ndani na nje ya nchi huku tukiamini tunaenda kuongeza ajira na kuongeza masoko badala ya kupeleka nje ya nchi anaweza kutumia kile kiwanda kama sehemu yake ya kuuzia mazao yake,” amesema Awadhi

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Senyi Ngaga ametoa wito kwa bodi hiyo kutumia vizuri nafasi yao kuhakikisha wanatatua changamoto kubwa ya uhaba wa masoko ya mazao ya wakulima.

“Siku zote tumekuwa tukilia kuhusu masoko tunazalisha ila hatujui wapi kwa kupeleka lakini tumesikia kutoka kwenu kwamba mnakuja kutatua changamoto hii kwa hiyo nawaomba wananchi kuongeza uzalishaji wa mazao,” amesema Ngaga

Akitoa maoni yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, Mandia Kihiyo ameiomba bodi hiyo kuwafikia wakulima katika maeneno yao na kuwapa elimu kuhusiana na fursa za kuhifadhi mazao yao kwenye maghala ya CPB na fursa za kuuza mazao yao ili kuongeza chachu ya uzalishaji.

“Tunaomba wenzetu wa bodi ya CPB tusaidie katika eneo hilo la utoaji elimu ili fursa zilizopo kwenye bodi yenu wakulima waweze kuzifahamu na kunufaika nazo lakini pia wapatiwe elimu elekezi kuhusiana na kiwango cha bei za bidhaa mbalimbali,” amesema Kihiyo

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Rock City Native, Yahya Callion ametoa wito kwa bodi hiyo kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanasimamia vizuri sheria za nchi na kuhakikisha wanunuzi kutoka nje ya nchi hawanunui mazao kimagendo kwa wakulima akidai wengi ununua yakiwa bado shambani.

“Kuna mazao mengi yanayopotea kupitia mitumbwi ambayo yanasafirishwa kwenda nje ya nchi na moja wapo ya sababu inayopelekea kuwa hivyo ni  wafanyabiashara hao kwenda moja kwa moja vijijini kule ambako wapo wakulima kisha kununua mazao kimagendo, naomba bodi kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha mnalidhibiti hili,” amesema Callion