Bosi CRDB aibuka kidedea tuzo za watendaji wakuu wa taasisi

Saturday October 09 2021
crdbpic
By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela ameibuka kinara katika tuzo za watendaji wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali na binfasi, zilizoandaliwa na taasisi ya Eastern Star Consulting Group Ltd.

Utoaji wa tuzo hizo, ulifanyika jana Oktoba 8, 2021 Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo  na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zanzibar, Omar Said Shaaban.

Tuzo hizo zinafanyika kwa mara ya kwanza nchini na zina lengo la kuhamasisha watendaji wakuu kuendelea kufanya kazi kwa bidii, licha ya mwaka jana dunia kukumbwa na ugonjwa Uviko-19, lakini baadhi ya kampuni ziliweza kutumia changamoto ya ugonjwa huo na kuzigeuza kuwa fursa.

Nsekela ameshinda katika kipengele cha ofisa mtendaji bora wa mwaka wakati Siaphoro Kishimbo wa CRDB akishinda kipengele cha ofisa mkuu wa rasilimali watu wa mwaka, huku Fredirick Nshikanabo wa benki hiyo, akiibuka kidedea katika ofisa mkuu wa fedha wa mwaka.

Pia CRDB imeshika nafasi ya nne katika kipengele cha ofisa biashara mkuu wa mwaka, huku Jared Awando, ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya bima ya Ice-Lion akishinda kipengele cha ofisa mwendeshaji mkuu wa mwaka.

Akizungumzia tuzo hiyo, Nsekela alisema, “tuzo hii ina watu nyuma waliochangia kuibuka kinara, kwanza ni mke wangu na familia yangu. Tuzo hii inaeleza namna CRDB iliyokuwa familia na kuwa kitu kimoja, nawaahidi tuzo hii itaendelea kubaki ndani benki hii,”amesema Nsekela.

Advertisement

Kwa upande wake, Kishimbo amesema huwezi kufanikiwa bila kufanya kazi kwa ukaribu na viongozi na wafanyakazi wengine. Wakati Kishimbo akieleza hayo Nshikanabo amewashukuru wafanyakazi wa CRDB kwa ushirikiano wao, akisema bila wao asingefanikiwaa.

 Mkurugenzi Mkuu wa Eastern Star Consulting Group Ltd, Alex Shayo amesema, “lengo la tuzo kuwatambua waliofanya vizuri.Mtu akifanya kazi nzuri atunukiwe na kupongezwa.

Advertisement