BoT inavyokalia mabilioni ya walalahoi wanaopoteza simu

BoT inavyokalia mabilioni ya walalahoi wanaopoteza simu

Muktasari:

  • Kati ya Oktoba 2019 mpaka Januari mwaka huu, zaidi ya wateja milioni 1.78 wa Mpesa walifungiwa akaunti zao zilizokuwa na Sh9.09 bilioni. Fedha hizi zilipelekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mujibu wa sheria.

  



Kati ya Oktoba 2019 mpaka Januari mwaka huu, zaidi ya wateja milioni 1.78 wa Mpesa walifungiwa akaunti zao zilizokuwa na Sh9.09 bilioni. Fedha hizi zilipelekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mujibu wa sheria.

Tofauti na kampuni nyingine za mawasiliano nchini, Vodacom imeweka utaratibu wa kupeleka orodha ya akaunti za Mpesa ambazo hazijatumika kwa muda mrefu BoT kila baada ya miezi mitatu.

Akaunti hizi zinazofungwa ni zile ambazo hazijatumika kwa muda mrefu kutokana na maradhi ya muda mrefu ya mteja husika, wizi, ajali au safari ya nje ya nchi ambako hakuna mtandao wa huduma.

Hata hivyo, wananchi wengi wamekuwa wakihangaika kurudisha fedha zao, jambo lililomshawishi Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kufanya uchunguzi maalumu wa usimamizi wa mali zilizookotwa au zisizo na mwenyewe (unclaimed assets).

Richard Mahinya, mkazi wa Lindi mjini anasema “ni shughuli kubwa kurudishiwa fedha zako. Niliwahi kupoteza simu na laini ikafungiwa, nilipojaribu kufuatilia salio langu, nilipewa mlolongo mrefu mpaka nikakata tamaa.”

Kwenye ripoti yake ya ukaguzi mwaka huu, CAG anasema mpaka Oktoba 2020, kampuni zote nne za mawasiliano zinazotoa huduma za fedha ziliwasilisha BoT jumla ya Sh12.6 bilioni zilizokuwamo kwenye akaunti za wateja wao. Kila kampuni ilipeleka orodha ya wateja pamoja na kiasi kilichomo kwenye akaunti.

Hata hivyo, katika ukaguzi wake, CAG anasema aliiona orodha ya wateja wa Ezy Pesa pekee, huku zaidi ya asilimia 75 kikiwa kimekaa kwa zaidi ya miaka mitano.

Katika ukaguzi alioufanya, anasema akaunti isiyotumika chini ya miaka mitano hutozwa ada ya Sh600. “Hii inadhihirisha kwamba, iwapo ufuatiliaji ungefanyika, ungethibitisha kiasi halisi kilichomo kwenye kampuni hizo,” anasema CAG.

Udhaifu wa Sheria

Kwa mujibu wa Kifungu cha 31 cha Kanuni za Mifumo ya Malipo ya Kidijitali za mwaka 2015, kikisomwa pamoja na Kifungu cha 56(3) cha Sheria ya Mifumo ya Taifa ya Malipo ya mwaka 2015 kinazitaka kampuni za simu kuzitambua akiba zilizomo kwenye akaunti za wateja wao ambazo hazijatumika kwa miaka mitano kama mali iliyotelekezwa.

“Changamoto iliyopo katika uwasilishaji wa akiba za wateja ni maelekezo ya BoT kutoeleweka vyema. Barua ya BoT haijaeleza wazi ni mara ngapi taarifa hiyo iwasilishwe kwa mwaka wala utaratibu wa kuwatambua wateja wasiotumia akaunti zao,” anasema CAG.

Uukiacha Mpesa iliyoahidi kuendelea kuwasilisha taarifa na fedha husika, kampuni nyingine hazikufanya hivyo tangu zilipoelekezwa Septemba 25 mwaka 2019. “Linaweza lisiwe tatizo kwa sasa, lakini huko mbele yanaweza yakajitokeza malalamiko mengi au Benki ikashtakiwa kwa kuzishikilia fedha za watu kwa muda mrefu,” wameeleza wafanyakazi wa BoT .

Ugumu kupata fedha

Ingawa BoT inakusanya fedha za wananchi kutoka kampuni zote za mawasiliano, haina utaratibu wa kuzirudisha kwa wahusika.

Benki hiyo haijaweka utaratibu wa mhusika au warithi kudai akiba yake hivyo kumaanisha fedha zikishaenda BoT huwezi kuzipata tena. “BoT haijaweka wazi utaratibu wa mwananchi kuzipata fedha zake, ingawa inasema fedha hizo inaendelea kuzitunza na haina mamlaka ya kuzitumia. Hata hivyo, inasubiri utaratibu wa kisheria kuwaruhusu wananchi kuzidai,” amesema CAG.

Kutokana na kutokuwa na utaratibu wa kuzitoa fedha hizo, BoT imeendelea kuzishikilia Sh12.6 bilioni kwa zaidi ya miaka mitano tangu mwaka 2015.

Tofauti na maoni ya CAG, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bernard Dadi anasema upo utaratibu wa kurejesha fedha za mteja.

Ikipita miezi sita ila chini ya miaka mitano bila mteja kuitumia, anasema huhesabika kama akaunti mfu (dormant account) na mtoa huduma anaweza kuiuza laini kwa mtu mwingine, lakini fedha zilizomo bado zinaendelea kuhesabika kuwa ni zake.

“Ikizidi miaka mitano huwa tunazipeleka fedha hizo kwenye mfuko wa Serikali kama found properties (mali ya kuokota) iwapo mwenyewe hajajitokeza, akijitokeza anarudishiwa. Wengi tu wamerudishiwa. Ukiwa na vithibitisho vyote, unaenda wizarani na unaandikiwa cheki,” anasema.

Tatizo lililopo, Dadi anasema ni kiasi kidogo kinachokuwapo kwenye simu ambacho kinawakatisha tamaa wengi kufuatilia utaratibu uliowekwa, hivyo kuziacha fedha zao zikienda serikalini.

“Wengi hawafuatilii kutokana na akiba inayokuwamo kuwa ndogo kwani nyingi ni kati ya Sh20,000 na Sh100,000, sasa wakilinganisha gharama zilizopo wanaona bora waache tu,” anasema.


Serikali yatoa neno

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba anasema akiba inayokutwa kwenye simu hupelekwa serikalini ikipita miaka mitano, lakini kuna maboresho yanafanyika.

“Kulikuwa na proposal (pendekezo) kwamba fedha za kwenye simu zitolewe ndani ya miaka mitano, ila tukasema ufanyike utafiti kupata uzoefu kutoka mataifa mengine. BoT inasimamia hilo,” anasema Tutuba.

Licha ya muda, pendekezo jingine lililotolewa anasema ni kuanzisha mfuko maalumu utakaokuwa unaratibu uwekezaji wa fedha zinazokusanywa kutoka kwenye akaunti za simu.

Ili kupata fedha za mteja ambaye hajaitumia akaunti yake kwa muda mrefu, Tutuba anasema kuna namna mbili. Kwanza ni mmiliki mwenyewe au mrithi wake.

Kwa mmiliki, anasema utaratibu unaanzia kwenye kampuni ya simu ambayo ikijiridhisha mteja atapelekwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambao watampa kibali cha kwenda BoT akalipwe fedha zake.

Iwapo anayefuatilia ni mrithi, anasema ataanzia mahakamani ambako akishathibitishwa atamalizia utaratibu uliobaki.

“Changamoto iliyopo ni kwamba watu wengi huwa hawatoi taarifa ya akiba waliyonayo kwenye simu zao, hivyo wakifariki warithi hawafuatilii. Kwa mazingira haya hakuna namna fedha zitarudishwa kwa sababu hakuna anayezidai,” anasema Tutuba.

Wakati katibu mkuu akisema utaratibu unaihusisha TCRA, mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Jabir Bakari anasema hilo ni jukumu la BoT, kwani wao wanahusika na mawasiliano tu.

“Kwenye kampuni za simu kuna huduma za mawasiliano na hizo za fedha. Masuala yote ya fedha yanasimamiwa na BoT wanaotoa leseni na maelekezo mengine sisi tunahusika na technical issues (masuala ya kitaalamu) tu. Sheria na miongozo yote kuhusu huduma za fedha iwe benki au kampuni ya simu wanaohusika ni BoT,” anasema Dk Bakari.