Brela kutoa elimu wamiliki manufaa
Afisa usajili wakala wa usajili biashara na leseni (Brela), Gift Raphael akizungumza wakati wa kikao cha majadiliano kuhusu utekelezaji wa kanuni za wamiliki manufaa baina ya wakala na vyombo vya uchunguzi.
Muktasari:
- Brela imesema kutokana na sheria mpya ya watumiaji wa taarifa za wamiliki manufaa itaendelea kutoa elimu kuwafikia wengi ili kujua umuhimu na athari zake na kufikia malengo ya Taifa.
Mbeya. Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) imesema itaendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa taarifa za wamiliki manufaa ili kuziwesha kampuni kuwasilisha taarifa zao.
Kauli hiyo imetolewa jijini hapa na Mkuu wa Idara ya Usajili wa Makampuni, Isdor Nkindi wakati wa kikao cha majadiliano kuhusu utekelezaji wa kanuni za wamiliki manufaa baina ya wakala na vyombo vya uchunguzi.
Nkindi amesema kutokana na sheria hiyo kuwa mpya na wengi kutoifahamu wanatarajia kuzifikia kampuni mbalimbali kuhakikisha wanatoa taarifa za wamiliki manufaa ili kutoathiri shughuli zao.
“Awali, Serikali ilitoa miezi sita lakini mwitikio umekuwa mdogo hadi kuondoa ukomo wake, hivyo Brela kama chombo chenye mamlaka tutaendelea kutoa elimu kuhusu sheria hii ambayo ni mpya,” amesema.
“Kwa sasa kinachofanyika ni faini kwa wanaojisajili nje ya muda kwa Sh2,500 na madhara ya kutowasilisha taarifa hizi ni iwapo milango itafungwa inamaana utaanza upya na itaathiri shughuli,” amesema Nkindi.
Amesema Brela imekuwa ikifanya maboresho mbalimbali ya kisheria na mifumo kutokana na kuthamini mchango wa makampuni kwenye kuchangia uchumi wa nchi, huku akikemea baadhi ya kampuni zinazokwepa kodi.
“Sheria ya kampuni sura ya 212 ilifanyiwa marekebisho kupitia sheria ya fedha 2020 kwa kuleta dhana ya umiliki manufaa wa kampuni, marekebisho yaliendana sambamba na utungwaji kanuni za wamiliki manufaa mwaka 2021 kusimamia ukusanyaji na utoaji taarifa manufaa wa kampuni,” amesema Nkindi.
Kwa upande wake Afisa msajili (Brela), Gift Raphael amesema wanatarajia kukusanya maoni na ushauri kwa ajili ya maboresho ya utekelezaji wa kanuni za wamiliki manufaa ili kuboresha utendaji kazi wao.
“Hata hivyo kumekuwa na maombi machache kutoka mamlaka zinazoidhinishwa kupata taarifa hivyo tunaamini kupitia warsha hii ili kuelimishana na kujengana kiuwezo katika shughuli zetu,” amesema Gift.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho, Boniface Tweve ambaye ni mwanasehria wa kujitegemea amesema elimu hiyo imewafungua akili kujua umuhimu wa mmiliki wa kampuni kutoa taarifa zake bila kutajwa majina.
“Hii itasaidia kuondoa mgongano wa kimaslahi kwani mmiliki anaweza kuwa na kampuni lakini asitajwe majina yake, japokuwa atatoa taarifa zake kwa vyombo vya kisheria kwa nia njema,” amesema Tweve.