Watakiwa kutumia huduma za Brela
Mfanyabiashara wa mjini Musoma, Raymond Malima (kulia) akipata maelezo kutoka kwa ofisa leseni wa Brela, Rajab Chambega kwenye maonesho ya biashara ya Mkoa wa Mara yanayoendelea mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
Wafanyabiashara nchini wametakiwa kuachana na vishoka wanapohitaji kupata huduma za Brela badala yake watumie njia sahihi ili kuepuka gharama zisizokuwa za lazima.
Musoma. Wafanyabiashara nchini wametakiwa kutumia huduma zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) badala ya kutumia njia zisizo sahihi kama vile ya mtu kati maarufu vishoka nnia ambazo zimekuwa ni mzigo kwao.
Wito huo umetolewa mjini hapa leo Jumamosi Septemba 3, 2022 na afisa leseni kutoka Brela, Rajab Chambega alipokuwa akizungumza na Mwananchi kwenye maonesho ya biashara ya mkoa wa Mara yanayoendelea mjini hapa.
Amesema kuwa tatizo la vishoka ni kubwa ingawa hakuweza kutoa takwimu na kwamba hali hiyo imekuwa ikifanya wafanyabishara wengi kuingia gharama kubwa bila sababu pale wanapohitaji kupata huduma za Brela.
"Siwezi kutoa takwimu kwa sasa lakini kuna watu wanajiita business consultant’s (washauri wa biashara) ambao wamekuwa wakitoza hela kubwa sana kwa watu wanaohitaji huduma zetu jambo ambalo sio sawa tunawaomba wafanyabiashara na watanzania wafuate njia sahihi," amesema.
Ametolea mfano wa Sh150, 000 ambazo wafanyabiashara wamekuwa wakitozwa kama gharama ya kusajili jina la biashara badala ya Sh20, 000 inayotozwa na wakala huyo.
Ili kuondokana na tatizo hilo amesema kuwa zipo jitihada kadhaa ambazo zimefanywa na wakala huyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya njia zipi zinatakiwa kufuatwa na wafanyabiashara pale wanapotaka kupata huduma Brela.
"Huduma zetu zipo kwenye mfumo kwahiyo ukihitaji kitu chochote unatakiwa kuingia kwenye mtandao na kwa wale ambao wanapata shida kuingia kwenye mfumo au mtandao tumetoa meelekezo kwa maafisa biashara wa mikoa yote kwahiyo wakifika kwa maafisa biashara watapata huduma zetu kwa gharama sahihi kabisa," amesema
Baadhi ya wafanyabiashara wameomba huduma za wakala huyo kusogezwa hadi ngazi ya wilaya kuliko hivi sasa ambapo wamekasimisha majukumu yao kwa maafisa biashara wa mikoa.
"Kuna unafuu kwa sasa tofauti na zamani ambapo mtu alikuwa anatakiwa kusafiri hadi Dar es salaam, ila sasa badala ya kupatikana kwenye kanda au ofisi za maafisa biashara wa mikoa Brela inatakiwa kufungua ofisi ngazi ya mikoa na halmashauri ili kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi," amesema Raymond Malima mfanyabiashara wa Musoma
Malima amesema kuwa suala la huduma kutolewa kupitia kwenye mtandao bado ni changamoto kwani maeneo mengi nchinj bado hayajawa na mtandao wa uhakika hivyo huduma za moja kwa moja kutoka kwa afisa wa Brela ni ya muhimu zaidi.
Mfanyabiashara mwingine, Editha Ntabaza amesema kuwa ili kuepukana na vishoka Brela inatakiwa kutoa elimu zaidi hasa mikoani ambapo watu wengi bado hawana taarifa sahihi kuhusu Brela na huduma zake.