Prime
Muhimbili yaanza upandikizaji titi wakitumia mwili wa mgonjwa
Muktasari:
- Wakati Tanzania ikianza matibabu hayo, katika nchi zilizoendelea upandikizaji au utengenezaji wa titi kwa kutumia mwili wa mgonjwa ni sehemu ya matibabu ya saratani ya matiti.
Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanza kutoa huduma ya upasuaji wa kutengeneza titi upya kwa wanawake waliopoteza titi kutokana na ugonjwa wa saratani au ajali, hatua inayotarajiwa kuboresha ubora wa maisha ya waathirika na kupunguza athari za kisaikolojia.
Mpaka sasa, wanawake wanne wamepatiwa huduma hiyo kupitia kambi ya madaktari iliyoanza Jumatatu wiki hii.
Huduma hiyo mpya inatekelezwa kupitia ushirikiano kati ya madaktari bingwa wa Muhimbili na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha California, San Francisco (UCSF), nchini Marekani, huku lengo likiwa si tu kuwatibu wagonjwa, bali pia kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani ili huduma hiyo iendelee kutolewa na Watanzania wenyewe.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili leo Alhamisi, Julai 2, 2026, Mkuu wa Idara ya Upasuaji, Dk Ibrahim Mkoma, amesema hospitali imeanzisha huduma hiyo kutokana na ongezeko la wagonjwa wa saratani ya matiti, ambao wengi hulazimika kuondolewa titi moja au yote mawili ili kuokoa maisha yao.
Amesema saratani ya matiti ni miongoni mwa saratani zinazoongoza kwa wanawake nchini, na wagonjwa wengi wanaofika Muhimbili hulazimika kufanyiwa upasuaji wa kuondoa titi kutokana na hatua ya ugonjwa.
"Kwa miaka mingi, wanawake hawa walikuwa wanaondoka hospitalini wakiwa wamepona saratani, lakini wamepoteza sehemu muhimu ya mwili wao. Sasa tunaanza kutoa huduma ya kurejesha mwonekano wa titi kwa kutumia tishu za mwili wa mgonjwa mwenyewe," amesema.
Dk Mkoma amesema kambi maalumu ya upasuaji ilianza Jumatatu na itaendelea hadi Ijumaa, na madaktari wa Tanzania na Marekani wanafanya upasuaji wa pamoja huku wakibadilishana uzoefu.
Amesema wagonjwa walifanyiwa uchunguzi wa awali katika kliniki na kuchaguliwa kulingana na vigezo vya kitabibu ili kuhakikisha wanaweza kufanyiwa upasuaji huo kwa usalama.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji Rekebishi Muhimbili, Dk Laurean Rwanyuma, upasuaji huo haufanywi kwa madhumuni ya urembo, bali ni sehemu muhimu ya ukamilishaji wa matibabu ya saratani ya matiti.
Amesema mwanamke anayepoteza titi hupitia changamoto kubwa za kisaikolojia, hupoteza kujiamini na, wakati mwingine, huathirika katika maisha ya familia na kijamii.
"Lengo la upasuaji huu ni kumrudishia mgonjwa utimilifu wa mwili na ubora wa maisha. Tunazungumzia kurejesha hali ya kawaida baada ya kumaliza matibabu ya saratani, si suala la urembo pekee," amesema.
Dk Rwanyuma amesema wagonjwa 18 walifanyiwa tathmini katika kambi hiyo, lakini sita pekee walikidhi vigezo vya kufanyiwa upasuaji baada ya kukamilisha matibabu ya saratani na vipimo vinavyohitajika.
Amesema wagonjwa wengine wataendelea kufuatiliwa hadi watakapokidhi masharti ya kitabibu.
"Tunawajengea uwezo wataalamu wetu ili baada ya ushirikiano huu, huduma ziendelee kutolewa hapa Muhimbili bila kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi," amesema.
Daktari bingwa bobezi wa upasuaji rekebishi, Dk Frank Mwamba, amesema takwimu za Muhimbili zinaonesha ukubwa wa changamoto ya saratani ya matiti nchini.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2024, hospitali ilipokea takribani wanawake 500 wenye saratani ya matiti, huku zaidi ya 200 wakifanyiwa upasuaji wa kuondolewa titi kutokana na ugonjwa huo.
"Hizi ni takwimu za Muhimbili pekee. Ukijumlisha hospitali nyingine nchini, idadi ya wanawake wanaopoteza matiti kila mwaka ni kubwa zaidi," amesema.
Dk Mwamba amesema upasuaji huo unafanyika kwa kutumia sehemu ya mwili wa mgonjwa mwenyewe, ambapo tishu kutoka maeneo yenye ziada huhamishwa na kutumika kutengeneza titi jipya.
Amesema, tofauti na matumizi ya vipandikizi vya bandia pekee, mbinu hiyo hutumia tishu hai za mgonjwa, ambazo huendelea kuwa sehemu ya mwili wake.
"Binadamu ana maeneo yenye tishu za ziada ambayo yanaweza kutumika kurejesha sehemu iliyopotea. Hiyo ndiyo teknolojia tunayotumia katika upasuaji huu," amesema.
Amesisitiza kuwa wanawake waliomaliza matibabu ya saratani na kuondolewa titi wasisite kufika katika Kliniki ya Upasuaji Rekebishi ya Muhimbili ili kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu chaguo walizonazo.
Kwa mujibu wake, kliniki hiyo hufanyika kila Alhamisi kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana.
Akijibu swali kuhusu gharama za huduma hiyo, Dk Mkoma amesema hospitali bado inafanya tathmini ya kina kabla ya kutangaza gharama rasmi kutokana na matumizi ya vifaa maalumu, utaalamu wa hali ya juu na muda mrefu unaohitajika wakati wa upasuaji.
Amesema mgonjwa anayefaa kufanyiwa upasuaji huo ni yule aliyekamilisha matibabu yote ya msingi ya saratani, kwani lengo kuu ni kuhakikisha ugonjwa umetibiwa kabla ya kuanza hatua ya kurejesha mwonekano wa mwili.
Kwa upande wake, daktari bingwa wa upasuaji rekebishi kutoka Chuo Kikuu cha California, San Francisco, Dk Edward Miranda, amesema wanawake wengi wanaopona saratani ya matiti huendelea kuishi kwa miaka mingi, hivyo kurejeshewa titi kunachangia afya ya akili, kujiamini na ubora wa maisha.
Amesema katika ziara yake ya kwanza Muhimbili alibaini hitaji kubwa la huduma hiyo, jambo lililosababisha kuanzishwa kwa mpango wa miaka miwili wa mafunzo kwa madaktari wa Tanzania.
"Upasuaji wa kurejesha titi ni sehemu muhimu ya matibabu kamili ya saratani ya matiti. Si kila mwanamke atahitaji huduma hii, lakini kwa wanaoihitaji imeonekana kisayansi kuboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa," amesema.
Ameongeza kuwa maendeleo yaliyofikiwa na timu ya madaktari wa Muhimbili yanaonesha kuwa huduma hiyo sasa inaweza kuendelea kutolewa nchini huku wataalamu wa ndani wakiongoza matibabu hayo.