Bugando yapata mashine ya kwanza ya uchunguzi wa saratani ya matiti

Mkurugenzi wa huduma ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Tamisemi, Dk Ntuli Kapologwe (wa tatu kulia) akisikiliza maelezo kuhusu mashine ya kufanya uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti kutoka kwa  mtaalam wa mionzi Bugando, Dk Margreth Magambo (hayupo pichani). Mashine hiyo imegharimu Sh800 milioni. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) leo wamekabidhi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando mashine ya kisasa ya kufanya uchunguzi wa awali na matibabu ya saratani ya matiti yenye thamani ya Sh800 milioni.

Mwanza. Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) leo wamekabidhi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando mashine ya kisasa ya kufanya uchunguzi wa awali na matibabu ya saratani ya matiti yenye thamani ya Sh800 milioni.

Mashine hiyo ambayo ni ya tatu katika nchi za Afrika Mashariki na ya pili nchini imenunuliwa na kutolewa chini ya mradi mtambuka wa saratani nchini (TCCP) unaotekelezwa kwa miaka minne tangu mwaka 2020.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mashine hiyo katika Hospitali ya Bugando, Meneja wa mradi wa TCCP, Dk Harrison Chuwa amesema mradi huo unalenga kuboresha vifaa tiba vya saratani, kuendeleza matibabu, kutoa elimu kwa watoa huduma ya afya na kufanya utafiti wa saratani nchini.

"Mradi huu unatekelezwa katika halmashauri za wilaya nane za Mwanza na tano za Mkoa wa Dar es Salaam ambapo utatoa huduma ya matibabu ya saratani kwa watanzania," amesema Dk Chuwa

Ametaja vifaa vitakavyonunuliwa kupitia mradi huo kuwa ni Mashine ya Ultrasound, mashine ya uchunguzi wa awali wa saratani, mashine mbili za kutoa tiba ya ndani ya mionzi zitazowekwa taasisi ya saratani ya Ocean Road na mashine mbili za mionzi ya nje zitakazosimikwa kwenye hoapitali ya Aga Khan na mashine gandishi za kubaini dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi zitakazosimikwa katika hospitali za wilaya katika mikoa hiyo.

Mkuu wa Idara ya Mionzi wa hospitali ya Aga Khan, Profesa Ahmed Jusabani amesema mashine hiyo ina uwezo wa kufanya uchunguzi wa saratani kwa watu 20 hadi 25 kwa siku.

Amesema mashine hiyo iliyosimikwa Bugando itasaidia kubaini dalili za saratani ya matiti huku akiwaomba wakazi wa Kanda ya Ziwa kujitokeza kufanya uchunguzi wa magonjwa hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa huduma za afya, Ustawi wa jamii na lishe Tamisemi, Dk Ntuli Kapologwe ameishukuru AFD na AKDN huku akiwaagiza waganga wakuu wa mikoa na Halmashauri nchini kutenga fungu la fedha kwa ajili ya kuwezesha kampeni ya kuhamasisha wananchi kufanya vipimo vya saratani.

 "Mwitikio wa kupima saratani bado ni mdogo hivyo ninawaagiza waganga wakuu nchini kuhakikisha wanatenga fedha kwenye bajeti zao kwa ajili ya uhamasishaji wa jamii juu ya upimaji ili kutokomeza saratani nchini nikitolea mfano saratani ya kizazi ambayo tumejiwekea malengo ya kuiondoa kufikia 2030," amesema Dk Kapologwe