Bunge lakipa kisogo Kiswahili


Muktasari:

  • Wakati lugha ya Kiswahili ikipitishwa na kupigiwa chapuo kutumika katika Jumuiya za Kimataifa, jana kiingereza kimeendelea kutumika katika uchaguzi wa kuwapata wabunge wapya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala).


Dar es Salaam. Wakati lugha ya Kiswahili ikipitishwa na kupigiwa chapuo kutumika katika Jumuiya za Kimataifa, jana kiingereza kimeendelea kutumika katika uchaguzi wa kuwapata wabunge wapya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala).

Machi 16 hadi 17, kwa mara ya kwanza Kiswahili kilitumika katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Pia Kiswahili kimepitishwa na Umoja wa Afrika (AU) kuwa lugha rasmi ya kikazi, huku ikiendelea kuzungumzwa katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki na jamii za waswahili katika Umoja wa Falme za Kiarabu na Oman.

Mwaka 2019, Baraza la mawaziri nchini Uganda lilikamilisha mpango wa Kiswahili kuwa lugha ya Taifa nchini humo na kutangaza kitumike kwenye Shirika la ndege la nchi hiyo.

Kama hiyo haitoshi, mwaka 2021, alipolihutubia Bunge la Kenya, Rais Samia Suluhu Hassan aliupongeza mhimili huo kwa kuazimia kutumia lugha ya Kiswahili.

Pamoja na juhudi za kukiendeleza Kiswahili, jana katika uchaguzi wa Eala, lugha ya kiingereza ilitumika kwa wagombea kujieleza, kujinadi na kuomba kura, huku wabunge hao wakiwauliza maswali kwa lugha hiyo, mchakato uliofanyika katika kikao cha Bunge kilichofanyika jijini Dodoma.

Kabla ya wagombea hao kuitwa, Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi alisema kwa mujibu wa kanuni ya 10 ya mchakato huo, kila mgombea ataruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge kujieleza na kujibu maswali kwa lugha ya kiingereza kadiri watakavyokuwa wakiulizwa na wabunge kwa maelekezo ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Hata hivyo, matumizi ya lugha hiyo yalionekana kuwapa wakati mgumu baadhi yao ya wagombea katika kujieleza, licha ya wengine kufanya vizuri.

Si wagombea pekee, bali hata waliouliza maswali, baadhi yao walijikuta wakikosea na kuibua vicheko bungeni.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ ni mmojawapo, aliibua vicheko kwa wabunge baada ya kumuuliza swali kwa Kiingereza mgombea wa nafasi hiyo, Habib Mnyaa.

Akiuliza swali kwa Mnyaa alisema, “thank you madame Speaker (Dk Tulia) for give me this chance, Mr Mnyaa I want to ask you one question, where are you, (ulikuwa wapi) what did you do for last five years? (ulikuwa unafanya nini ndani ya miaka mitano iliyopita), swali liliongeza vicheko zaidi kwa wabunge hasa waliokuwa wamekaa karibu na mbunge huyo na wengine wakimpigia makofi huku akionekana kutunzwa fedha za noti ya Sh10,000 na baadhi ya wabunge wenzake. Katika kuweka mambo sawa, Dk Tulia alinyoosha swali hilo kwa kusema ‘what did you do for past five years.’

Akijibu swali hilo Mnyaa alisema, “nilikuwa nafanya kazi katika Bunge Eala kupitia kamati na nilifanya vitu vingi, nikishirikiana na wenzangu katika miaka mitano iliyopita. Nasimama mbele yenu nikiomba kura zenu.

Swali la mbunge wa Lulindi, Ally Mchungahela kwa mgombea Thomas Malima unaweza kusema lilikuwa la kustaajabisha, aliuliza “Kanda hii imekuwa miongoni mwa dampo la soko. Je, una mikakati gani ya kupunguza tatizo hilo?”

Hata hivyo, Malima hakuweza kujibu swali hilo mara moja, bali aliomba lirudiwe. Dk Tulia alikubali swali hilo lilirudiwe, “Kanda hii ni miongoni mwa dampo la soko la nje. Una mikakati gani wa kupunguza tatizo la utupaji taka katika eneo hili la Jumuiya ya Afrika Mashariki? Hata hivyo, Spika aliingilia kati na kuliondoa swali hilo.


Wadau wa Kiswahili wakerwa

mtaalamu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Aldin Mutembei alisema kufanya hivyo si kujiaibisha pekee bali ni kujifedhehesha.

Alieleza vitendo hivyo ndivyo vinavyofanya juhudi za kupigania maendeleo ya Kiswahili zionekane zinafanywa kwa sababu watu hawajui Kiingereza.

“Tutaendelea kuonekana kwamba tunapigania Kiswahili kwa kuwa hatujui Kiingereza wakati si kweli. Kwa sababu wawakilishi na viongozi wetu wanaokwenda huko sio makini,” alisema. Kukosekana kwa umakini wa viongozi hao, alisema kunatokana na kushindwa kutumia vema lugha na kukosa utambulisho wanaousimamia.

Mhariri Mwandamizi wa lugha ya Kiswahili, Onni Sigala alisema uamuzi wa kutumia Kiingereza katika kampeni za bunge hilo haimaanishi kwamba Kiswahili kinadharauliwa.

Alisema pengine ndiyo lugha inayotumika katika shughuli za Bunge husika hivyo, inafanyika hivyo ili kutowanyima wengine wanaohitaji kujua kinachozungumzwa.Hata hivyo, kuamua kutumia lugha ya Kiingereza haimaanishi tunakidogosha Kiswahili, tunapotumia lugha hiyo katika mazingira ambayo yanawalazimu watu wengine wajue kinachozungumzwa ni kuwapa haki yao ya kusikia,” alisema.

Mhadhiri wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Aginiwe Sanga alisema licha ya umuhimu wa Kiingereza kutokana na ukubwa wake, hakuna haja ya kujilazimisha kukitumia katika mazingira ambayo Kiswahili kinaeleweka zaidi.

“Ni lugha inayotufanikisha mambo mengi, lakini pale penye tija mfano Afrika Mashariki si jambo zuri kujilazimisha kutumia Kiingereza wakati tunakuwa huru tukitumia Kiswahili na sisi wote tunakielewa,” alisema.