Bweni la wasichana Kilolo lateketea moto

Muktasari:

  • Bweni la wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari ya St Michael, Kijiji cha Luganga, Wilayani Kilolo mkoani Iringa limeteketea kwa moto na kusababisha hasara ya vitu.

Iringa. Wasichana wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Michael (St Michael) inayomilikiwa na Kanisa la Anglikana katika kijiji cha Luganga, Wilaya ya Kilolo, Kijiji cha Luganga wamenusurika baada ya bweni la limeteketea kwa moto.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa shule hiyo Gideon Malifimbo amesema hakuna mwanafunzi yeyote aliyejeruhiwa zaidi ya kupoteza vifaa vyao vya shule, nguo, magodoro na vitanda.

Amesema bweni hilo liliungua juzi, Januari 29 kuanzia saa 12.30 jioni huku chanzo kikiwa hakijulikani mpaka sasa.

Mkuu wa Jeshi la zima Moto Wilaya ya Kilolo, Isakwisa Mwakasangula amesema baada ya taarifa hiyo waliwahi na kufanikiwa kuuzima ili usiendelee kuleta madhara zaidi.

Kutokana na hali hiyo, walilazimika kuanza kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya moto na kuwataka wanafunzi kuzingatia matumizi sahihi ya umeme mabwenini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Peresi Magili amesema wanaendelea kuchunguza ili wajue chanzo cha moto huo.

"Nataka miundombinu ya mabweni ifanyiwe maboresho, tena shule hii mmenifungua macho nitafanya ziara za kushitukiza katika shule zote za Wilaya ya Kilolo kukagua miundombinu ya mabweni, " alisema Magili

Magilii amesema serikali ya Wilaya ya Kilolo itatoa msaada kwa vifaa mbalimbali vilivyoungua ikiwa ni pamoja na vitanda mashuka na magodoro.