Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bweni shule ya Makete laungua mara ya pili

Bweni shule ya Makete laungua mara ya pili

Njombe. Uongozi wa Wilaya ya Makete, unafanya uchunguzi kubaini watu waliohusika kuchoma moto bweni la wavulana katika shule ya sekondari Mang’oto iliyopo wilayani Makete mkoani Njombe.

Bweni hilo liliungua moto na kusababisha baadhi ya vitu vilivyokuwamo ndani kuteketea.

Akizungumza na Mwananchi jana mara baada ya kutembelea shule hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Makete, Veronica Kessy, alisema amesikitishwa na tukio hilo kwa kuwa bweni hilo liliwahi kuungua kwa kuchomwa moto na mwanafunzi mmoja shuleni hapo.

Alisema alipopata taarifa za kuungua kwa bweni hilo alipatwa na mfadhaiko, kwani Machi, 2018 bweni liliungua, huku juhudi zikifanyika kuchangisha wananchi na wadau ili kutoa fedha na kukarabati bweni hilo.

“Sasa katika kipindi cha miaka miwili bweni linaungua tena katika mazingira yaleyale, jambo ambalo linatia mashaka,” alisema Kessy.

Kamati ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na maofisa wa Serikali waliofika katika shule hiyo, katika hatua za awali walisimamia mchakato wa kuwabaini wahusika kupitia wanafunzi wa shule hiyo.

Baada ya kazi hiyo, kamati hiyo iliondoka na baadhi ya wanafunzi ili kufanya mahojiano zaidi na kupata ukweli juu ya chanzo cha kuungua kwa bweni hilo.

Kessy alisema hatua hizo ni za awali huku akiwataka wanafunzi kutoa ushirikiano kwa kuwapa taarifa walimu wao kama wanawafahamu watu waliofanya kitendo hicho.

“Kama kuna mtu mnamfahamu amefanya kitendo hicho mfuateni mwalimu wa malezi mkamwambie kwani itakuweka huru,” alisema Kessy.

Naye Ofisa elimu mkoa wa Njombe, Gift Kyando aliwaeleza wanafunzi hao kutambua wajibu wao wawapo shuleni na kujiepusha na mambo yasiyo na msingi.

“Hata ukikasirika lakini siyo kuchoma bweni au darasa, mmechoma bweni mara ya pili sasa wazazi wenu huko wanahangaika, inakuwaje mtu unachoma mahala pa kulala?” alihoji Kyando.