Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CAG alalama kuingiliwa uhuru wake akieleza madudu ya taasisi, Rais Mwinyi aagiza kuundwa kamati

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akipokea ripoti ya  Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Zanzibar kwa mwaka 2022/2023 kutoka kwa CAG, Dk Othman Abbas Ali. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Zanzibar amekabidhi ripoti ya ukaguzi kwa mwaka 2022/23 na kubainisha mambo mbalimbali.

Unguja. Licha ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Zanzibar, kuonyesha kuimarika kwa hati za ukaguzi, baadhi ya taasisi zimeendelea kuwa na dosari kubwa ya ufungaji wa hesabu kusababisha kuwa na hati zenye shaka au kushindwa kutoa maoni.

 Ripoti hiyo ya mwaka 2022/23 iliwasilishwa na CAG, Dk Othman Abbas Ali leo Jumatatu, Mei 13, 2024 Ikulu Zanzibar ambapo amesema licha ya kufanya maboresho ya hesabu hizo bado kuna changamoto kutokana na vigezo vya ufungaji wa hesabu.

Mbali na hati chafu, pia CAG ametaja kuwapo na mifumo ya Serikali ambayo haina ufanisi huku mingi ikikodiwa kutoka nje na kuwapo na uwezekano wa kusababisha uvujaji wa siri za Serikali na kushindwa kufikia malengo.

“Changamoto ninazokutana nazo ni kutikishwa uhuru wangu kikatiba katika kutekelza majuukumu yangu, kuna mmoja alisema ana nguvu kwani akija kwako saa nne asubuhi, saa nane naondoka katika nafasi hii,” amesema bila kumtaja jina.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza baada ya kupokea ripoti ya CAG. Hafla iliyofanyika leo Mei 13,2024 Ikulu, Unguja. Picha na Ikulu

Kadhalika, CAG ametaja changamoto anazokutana nazo ikiwa ni pamoja na kuingiliwa kazi zake kutoka kwa wateule wa Rais wakiwemo mawaziri wakimuelekeza anachotakiwa kufanya, hata hivyo bila kuwataja amesema alikaidi maagizo yao.

Wakati Dk Abbas akitoa hayo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka watendaji wanaoingilia kazi za CAG  kuacha mara moja kwa sababu yupo kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu kupunguza hoja za CAG, Dk Mwinyi amesema umefika wakati sasa kuwa na kamati maalumu ya kushughulikia hoja za kiutendaji zinazowasilishwa katika taarifa ya CAG na kumuagiza Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said kuunda kamati hiyo mara moja.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, hoja za kijinai ndizo zitakazopelekwa katika Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Rushwa na Uhujmu Uchumi (Zaeca) na za kiutendaji zitashughulikiwa.

Pia Dk Mwinyi amezitaka taasisi zilizoendelea kupata hati zenye mashaka na kushindwa kutoa maoni zijitathmini, kwani haiwezekani kila mwaka kuendelea kupata hati hizo. “Kwa sasa ziondolewe kabisa hizi taasisi haiwezekani kila mwaka zinapata hati chafu.”   

Hata hivyo, amesema anaridhishwa na ripoti hiyo kwani imeonyesha mafanikio na kupiga hatua ikilinganishwa na miaka iliyopita. 

Hati zilizotolewa

Jumla ya hati 165 zimetolea na kati ya hati hizo 138 zinaziridhisha, hati 12 zinashaka na hati 15 zilizoshindwa kutoa maoni ya ukaguzi.

Kwa upande wa Serikali Kuu hati 69 zilitolewa kati ya hizo  63 ni hati zinazoridhisha sawa na asilimia 95.45 ya hati zilizotolewa, huku tatu ni zenye shaka sawa na asilimia 4.5 ya hati zilizitolewa.

 Kwa upande wa mashirika ya umma na taasisi zinazojitegemea, jumla ya hati 45 zilitolewa, kati ya hizo 39 zinaliridhisha sawa na asilimia 86 ya hati zilzitolewa, huku sita ni zenye shaka sawa na asilimia 13.3 ya hati zilizotolewa.

Kwa upande wa tawala za mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, jumla ya hati 22 zilitolewa na kati ya hati hizo 19 zinaridhisha sawa na asilimia 86.36 na tatu ni zenye shaka sawa na asilimia 3.4 ya hati zote.

Katika miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), jumla ya hati 32 zimetolewa kati ya hizo 17 zinazoridhisha sawa na asilimia 53.3 na 15 za kushindwa kutoa maoni ya ukaguzi sawa na 46.8 ya hati zote.

Hati shaka

Ameitaja taasisi ambazo hati zake zina shaka kuwa ni  Hesabu Jumuishi ya mfuko Mkuu wa Serikali, Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Mamlaka ya usafiri Baharini (ZMA), Shirika la Miundombinu ya Tehama (Zictia), Wakala wa Karakana kuu ya Magari Zanzibar, Wakala wa Usajili na Mali.

Nyingine ni PBZ Mufindi Community Bank (Mukoba), Mfuko wa wa barabara, Baraza la Manispaa Mjini, Baraza la Manispaa Magharib B na Halmashauri ya Wilaya ya Kusini Unguja.

Hati kushindwa kutoa maoni

Akizungumzia miradi iliyoshindwa kutoa maoni ya ukaguzi amesema ni mradi wa kusaidia sekta za uchukuzi, mradi wa ujenzi wa bustani ya Mwanamashungi, mradi wa soko la machomanne, mradi soko la samaki mbogamboga Mkoani, mradi wa ujenzi kituo cha mabasi.

Mingine ni mradi wa umwagiliaji maji, uendeshaji takwimu Zanzibar, mradi wa kudhibiti upotevu wa mazao, mradi shirikishi afya ya uzazi na mama na mtoto, kutokomeza malaria Zanzibar, kudhibii VVU, Kifua kikuu na ukoma na mradi wa ujenzi wa barabara kuu. 

Hati hii hutolewa iwapo CAG anaposhindwa kupata ushahidi wa kutosha au taarifa muhimu kufikia malengo ya ukaguzi ikiwemo kutowasilisha nyaraka muhimu za ukaguzi, kuwekewa zuio la kukamilisha kazi za ukaguzi pamoja na kutokupewa ushirikiano wa kutosha.

Pia alitoa hati zenye shaka baada ya kujiridha kuwa taarifa za hesabu iliyoandaliwa na kuwasilishwa kuwa na makosa yanayoathiri mtiririko wa taarifa za fedha zilizowasilishwa, na madhara yaliyobainika ni makubwa.

CAG amewashauri maofisa masuhuli waongeze umakini na nidhamu katika usimamizi wa rasimali za umma.

Hata hivyo almesema mapendekezo 3,394 ya mwaka 2021/22 yaliyotolewa yalitakiwa kutekelezwa kutoka katika taarifa 170 za ukaguzi wa hesabu za mwaka jana.

Kati ya mapendekezo hayo 2,469 sawa na silimia 72.7 yalitekelezwa kikamilifu na mapendekezo 339 sawa na asilimia 9.99 yanaendelea kutekelezwa na mapendekezo 230 sawa na asilimia 6.7 hayakutekelezwa, huku mapendekeo 225 sawa na silimia 6.63 yamejirudia na mapendekezo 131 sawa na asilimia 3.4 yamepitwa na wakati.

Mifumo

Jitihada zaidi zinahitajika kuimarisha udhibiti wa mifumo ya ndani ikiwemo mikakati maalumu kwa maofisa masuhuli kuzifanyia kazi hoja za wakaguzi wa ndani kuepuka kujirejea.

Gawio

Dk Abbas amesema Serikali ilikadiria kupokea gawio la Sh32 bilioni kutoka mashirika mbalimbali, hadi kufikia Juni makusanyo yalikuwa Sh18.2 sawa na asilimia 56.

 Kwa mujibu wa CAG, kutofikiwa malengo kumechangiwa na mitaji midogo inayotumiwa na mashirika ya umma katika kujiendesha na mengine kujiendesha kwa mitaji hasi na kutegemea mikopo na ruzuku kutoka serikalini, kutomudu kuingia katika ushindani soko la kibiashara.

 Jambo lingine ni kutokana na madeni makubwa ya taasisi za Serikali zinazopatiwa huduma na mashirika ya umma, zinashindwa kulipa jambo ambalo Dk Mwinyi alisema tayari Serikali ilishatoa maelekezo kwamba kila taasisi illipe madeni hayo kadri wanavyotumia huduma hizo.

Ameshauri Serikali kwa mashirika yanayoweza kutoa gawio ili yaweze kupatiwa misamaha ya muda maalumu, ya utoaji gawio kwa Serikali kwa lengo maalumu kutoa nafasi kwa mashirika hayo kujipanga na kujiimarisha kibiashara kutokana na faida chache wanayoipata.

Deni la SMZ

Mwenendo deni la Serikali amesema kufikia Juni 2023 limefikia jumla ya Sh354.8 bilioni, la ndani ni Sh342.4 bilioni sawa na silimia 96 na deni la nje linalodhaminiwa na SMZ ni Sh13.3 bilioni sawa na asilimia 4 ya deni lote.

Deni la ndani la hati fungani ya muda mrefu zilifikia Sh159.5 bilioni, hati fungani maalumu za benki kuu Sh12 bilioni na mkopo wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ulifikia Sh61.9 bilioni.

Deni la nje linalodhaminiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Zanzibar limefikia Sh2.3 trilioni.

Dosari ukusanyaji mapato

Licha ya kuimarika ukusanyaji wa mapato bado kuna dosari zinazotokana na baadhi ya taasisi kukusanya mapato nje ya mfumo, mapato kutumika kabla ya kuwasilisha benki, ucheleweshaji wa mapato kuwasilisha sehemu husika na kupotea vitabu vya kukusanyia mapato na kutolingana hali halisi yanayokusanywa na yanaowasilishwa benki.

Pia, kutokuonyeshwa mapato halisi yaliyokusanywa katika hesabu za mwisho wa mwaka hivyo taasisi kushindwa kutekeleza kazi zake kwa ufanisi, kwa sababu ya watendaji kushikilia mapato mikononi pasi kuziwasilisha sehemu husika. 

Mifumo ya Tehama

Kwa mujibu wa CAG licha ya mifumo kuwa na umuhimu wake lakini inayotumika na Serikali ni ya kukodi, haina ufanisi jambo linalohatarisha usalama wa taarifa za Serikali kuvuja nje 

Ametolea mfano wa mfumo wa kufanya manunuzi ya Serikali ambao mfumo huo umekodiwa na kwa mwezi unalipiwa Sh500 milioni hivyo unatakiwa kulipiwa Sh31 bilioni kiasi ambacho ni kikubwa (bila kufafanua ni kwa muda gani).

Ameutaja mfumo mwingine ambao hauna uwezo ni  wa e-parking uliopo katika uwanja wa ndege, kwa mujibu wa CAG mfumo huo unapoteza mapato mengi ya Serikali kutokana na ufanisi wake mdogo.

Hospitali 11

Amesema katika ukaguzi wake, wakati wa ujenzi wa hospitali 11 za wilaya, kuna mzabuni aliyeshinda kwa kujenga kwa Sh17 bilioni lakini badala yake alipewa mwenye gharama za juu Sh24 bilioni.

Asilimia 10 za Halmashauri

Amesema katika ukaguzi wake, asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwenda kwa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) bado Sh955.5 milioni hazijapelekwa.

Dk Mwinyi 

Akizungumzia ripoti hiyo Dk Mwinyi ameagiza kila mmoja kwa eneo lake kuhakikisha changamoto hizo zinashughulikiwa na kuondoa hoja zote.

“Wakati umefika ripoti za CAG  ziwe  na mafanikio zaidi ya changamoto.”

Pia amesema ni marufuku taasisi za Serikali kuingia mikataba bila kuhusiha mwanasheria mkuu wa serikali.

“Pamoja na upungufu uliojiotekeza kwenye ripoti hii lakini mafanikio ni makubwa mno, hati safi za ukaguzi asilimia 95.4 ni mafanikio makubwa. Sasa umefika wakati wa kuwa na kamati maalumu ya kushughulikia hoja za kiutendaji,” alisema