Prime
Kibarua chamsubiri Majaliwa bungeni, ripoti za CAG yawaweka matumbo joto vigogo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Ni katika mkutano wa Bunge utakaoendelea kesho Jumatatu kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kujibu hoja tano zilizojadiliwa zaidi na wabunge wakati wakijadili bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2024/25
Dodoma. Si hoja ya fedha na hesabu pekee. Ni juu ya maisha halisi ya watu, ndoto zao na matumaini yao yanayosubiri majibu ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atakapokuwa na kibarua cha kujibu hoja tano zilizotolewa na wabunge wengi.
Kuna hoja nyingi zilizotolewa na wabunge wakati wakijadili taarifa kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/2025. Lakini, hoja tano zilizoonekana kurudiwa na wabunge wengi.
Waziri Mkuu aliwasilisha taarifa yake bungeni Jumatano ya Aprili 3, 2024 na ilipangwa kujadiliwa kwa siku tano, kuanzia Aprili 3 hadi Aprili 9, 2024.
Hata hivyo, ilishindikana kujadiliwa kwa siku zote hizo, kwanza kutokana na kifo cha Mbunge wa Kwahani, Kisiwani Zanzibar (CCM), Amed Yahya Abdulwakil, aliyefariki ghafla kwa tatizo la shinikizo la damu; na mwili wake kuzikwa jimboni mwake.
Kwa mujibu wa kanuni ya 173 ya uendeshaji wa Bunge inayohusu msiba wa mbunge, Jumanne ya Aprili 9 hakukuwa na kikao cha Bunge ili kutoa fursa kwa wabunge kushiriki msiba, pia Aprili 10-11 ilikuwa Sikukuu ya Idd El Fitri na Aprili 12-14 hakukuwa na Bunge hadi kesho Aprili 15 2024.
Baada ya kuhitimishwa kwa bajeti hiyo ya Waziri Mkuu, zitakazofuata kwa wiki hii ni Bajeti Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inayoongozwa na Mohamed Mchengerwa itakayojadiliwa kwa siku tatu kisha itafuatia Bajeti ya Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inayoongozwa na George Simbachawene ambayo hiyo inatajadiliwa kwa siku moja.
Hoja hizo tano zilizotolewa na wabunge zaidi ya mmoja ni kuhusu kanuni mpya ya kikokotoo, mawaziri kutoa ahadi hewa, tozo ya laini za simu ya Sh2,000 na Sh10,000 kuchangia bima ya afya, katikakatika ya umeme na mauaji ya watu kwenye hifadhi ikiwamo wananchi kuvamiwa na wanyama kama tembo, mamba na nyani.
Mfano, hoja ya kikokotoo ilitolewa na wabunge Ester Bulaya (Viti Maalum), Mrisho Gambo (Arusha Mjini), Kasalali Mageni (Sumve) na Florent Kyombo (Nkenge) ambao wote waliitaka Serikali kukaa na wafanyakazi na kuirejesha sheria hiyo bungeni.
Mbunge wa viti maalumu anayetokana na vyama vya wafanyakazi, Jane Jerry yeye alisema yawezekana elimu ya kikokotoo haijatolewa ipasavyo kuainisha faida na hasara kwa kuwa wafanyakazi wako gizani, hawaelewi wanacholipwa kimetokana na nini na kwamba elimu inahitajika.
Kinachopingwa na wafanyakazi ni kanuni mpya ya kikokotoo ya mafao ya mkupuko kuwa asilimia 35 badala ya asilimia 50 kama ilivyokuwa awali.
“Kuteleza si kuanguka, turudi tukae, tuwasikilize, hizi ni pesa zao Serikali inaweka, wapeni mafao kwa mkupuko kwa asilimia 50, hiyo nyingine muwape kidogo kidogo.
“Yale mafao ya mkupuo ndiyo yanayowasaidia, si hiki ambacho mnawapa kila mwezi, wakiweka misingi haya mengine yatakuwa ya kawaida,” alisema Bulaya.
Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni akichangia kuhusu kikokotoo alisema inawezekanaje mfanyakazi mwenye uzoefu wa kushika fedha na maisha akistaafu Serikali iamue kumtumzia fedha zake.
Kwa upande wake Gambo alitoa mifano ya jiinsi wastaafu wanavyopunjwa na kanuni mpya ya kikokotoo kwamba;
“Kwa yule ambaye mshahara wake kwenye kiwango cha wakurugenzi, labda milioni 3.720 (Sh3 milioni) kwa kikokotoo cha kabla ya Julai 2014 angepata milioni 266 (Sh266 milioni) kwa kikokotoo cha sasa angepata milioni 133 (Sh133 milioni) ambayo tofauti yake anakuwa amepunjwa milioni 135 (Sh135 milioni).”
Ahadi hewa za mawaziri
Pia, Waziri Mkuu Majaliwa atakuwa na kibarua cha kujibu hoja za mawaziri kutoa ahadi hewa iliyotolewa na mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni.
Mbunge huyo kwenye mchango wake alimtaka Waziri Mkuu kuwaeleza mawaziri waache kutoa ahadi hewa za ujenzi wa barabara katika Jimbo la Sumve, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Mageni aliwataja mawaziri wa ujenzi walioahidi bila kutekeleza kuanzia kwa Dk Leonard Chamuriho, Profesa Makame Mbarawa na sasa Innocent Bashungwa kwamba na yeye hakuna kitu alichokifanya na akiongea naye anamwambia kuwa michakato ya ununuzi inafanyika.
“Wakati anachangia bajeti yake ya pili, Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliniandikia memo kuwa watajenga barabara hiyo, lakini baadaye wakasema wanakopa na kwamba kila siku ni stori.
“Niko very serious, watu wa ujenzi, sitaki mchezo wananchi wa Sumve wanataka lami hawataki mchezo,” alisema Mageni.
Hoja ya barabara pia ilichangiwa na mbunge wa Ushetu (CCM), Emmanuel Cherehani aliyesema ubovu wa barabara nyingi nchini unatokana na usimamizi hafifu wa wakandarasi wanaozijenga.
Alisema katika maeneo mengine hata mvua ikinyesha kidogo tu, madaraja yanaenda ya maji au barabara zinachimbika.
Mauaji hifadhini
Pia, Waziri Mkuu atakuwa na kibarua cha kujibu madai ya mbunge wa viti maalumu, Esther Matiko aliyetoa vielelezo bungeni akithibitisha madai ya vitendo vya mauaji vinavyodaiwa kufanywa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) kwa wananchi walio jirani na hifadhi hiyo mkoani Mara.
Matiko alitoa madai ya kuwashutumu askari wa Senapa kwamba ndani ya kipindi kifupi wamefanya mauaji kwa raia wanaodaiwa kuingiza mifugo kwenye hifadhi.
Mbali na hayo, Matiko alidai ni miezi mitatu tangu awasilishe malalamiko hayo kwa katibu mkuu na waziri mwenye dhamana na Wizara ya Maliasili na Utalii, na hayajafanyiwa kazi.
Hata hivyo, Naibu Spika Musa Zungu alisema Matiko amewasilisha mezani kwake nyaraka za uthibitisho wa madai yake na aliitaka Serikali ije majibu kuhusiana na madai hayo.
Hoja ya Shabiby
Pia, mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby naye alikuja na hoja za kipekee akiishauri Serikali kukata Sh2,000 kila mwezi kwenye laini za simu za wananchi wa kawaida, huku laini za wabunge, wafanyabishara na wafanyakazi wakatwe Sh10,000 kwa mwezi fedha hizo ziwe chanzo cha mapato kwa Bima ya Afya kwa wote.
Kwa mujibu wa Shabiby nchini kuna wamiliki wa laini za simu milioni 72 ambao makato yao kwa mwaka yataingiza Sh1.720 trilioni na zikijumlishwa za Sh10,000 kwa mwezi za wabunge, wafanyabiashara na wafanyakazi Serikali itapata kwa mwaka takriban Sh2 trilioni, zitasaidia kuwa chanzo cha mapato ya uhakika kwa Bima ya Afya kwa wote.
Pia, Shabiby alitoa hoja nyingine akiishauri Serikali ibinafsishe hospitali, zahanati na vituo vya afya za vijiji na kuzitaja hospitali za rufaa pekee kama Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ndiyo zimilikiwe na Serikali.
“Korea Kusini hakuna hospitali ya kijijini ambayo ni ya Serikali, hakuna kituo cha afya ambacho ni cha Serikali, zahanati zote zimeingizwa kwenye mfumo mmoja, vituo vya afya vyote vimo kwenye mfumo mmoja,” alisema na kuongeza kuwa hoja ni kutokana na ukosefu wa uzalendo wa waliopewa majukumu kwenye hospitali hizo.
Hoja ya Shabiby ya kubinafsisha hospitali, zahanati na vituo vya afya pia iliungwa mkono na mbunge wa Musoma Mjini (CCM), Vedastus Manyinyi.
“Tunavyoelekea kwenye bima ya afya kwa wote mimi ushauri wangu hebu tuondoe kabisa Serikali kwa maana ya kuwa na vituo vya afya na zahanati. Na kwa sababu tutatumia bima ya afya ni vizuri, hivyo vituo vya afya, zahanati na hospitali tukayapa kwanza yale mashirika ya kidini ili yaweze kuhudumia, lakini tofauti ya hapo tuwape wa ‘private’ (binafsi).
“Maana tukiendelea kuwa sisi kama Serikali kuendesha maana yake ni kwamba zile huduma zitaendelea kuwa za hovyo ni kwamba ‘forgery’ (kughushi) nyingi zitaendelea kufanyika kutokana na zile bima za afya, nadhani haiwezi kusaidia,” alisema Manyinyi.
Vigogo matumbo joto
Mbali na kibarua cha Majaliwa, jambo jingine linalosubiriwa wiki hii ni vigogo serikalini kuwa na matumbo joto baada ya Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kwa mwaka 2022/23 itakapowasilishwa bungeni.
Ripoti hizo za CAG zitawasilishwa na Serikali baada ya CAG kuziwasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Machi 28, mwaka huu na kuonesha ubadhirifu wa maeneo mbalimbali kwenye taasisi za umma.
Tayari Rais Samia Aprili 4 mwaka huu, wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua wakiwamo mawaziri, alitoa maagizo kwa mawaziri wake juu ya ripoti ya CAG.
Aliwataka watendaji hao kwenda kuifanyia kazi ripoti hiyo na kujibu hoja zilizoibuliwa.
“CAG ametoa ripoti na katika ripoti yake amesema mambo kadhaa na hii ni kwa mawaziri wote, ripoti ya CAG ikasimamiwe ikafanyiwe kazi, hoja zijibiwe haraka. Mkijibu haraka tutaweza kujua yapi yamejibika na hatua gani zichukuliwe.”