CCM, Chadema waujadili utafiti wa Twaweza
Katibu MKuu wa Chadema, Vicent Mashinji akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.Picha na Said Khamis
Muktasari:
Ripoti ya utafiti huo iliyotolewa juzi ilibainisha kushuka kwa kiwango cha kukubalika kwa Chadema, lakini CCM inakubalika zaidi kwa wazee na watu wasiokuwa na elimu.
Dar es Salaam. Chadema imeeleza kushangazwa na vigezo vilivyotumiwa na utafiti wa Twaweza kwamba umaarufu wa vyama vya siasa vya upinzani umeshuka, wakati vyama hivyo vimepigwa marufuku kufanya siasa.
Ripoti ya utafiti huo iliyotolewa juzi ilibainisha kushuka kwa kiwango cha kukubalika kwa Chadema, lakini CCM inakubalika zaidi kwa wazee na watu wasiokuwa na elimu.
Utafiti huo ulibaini kuwa kukubalika kwa Chadema kumeporomoka kutoka asilimia 32 mwaka 2013 hadi asilimia 17 mwaka huu.
Chadema ilibainika kuungwa mkono na wasomi, vijana, wanaume, matajiri na wenye elimu ya kutosha.
Lakini, akizungumzia kuhusu utafiti huo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema hakubaliani nao kwa vile hauelezi ukweli wowote wa mambo.
Alisema Chadema imeshangaa kuona Twaweza inakuja na utafiti ili hali shughuli za vyama vya siasa zikipigwa marufuku na Serikali.
Kwa maana hiyo alidai utafiti huo hauwezi kukubalika kwa vile haujaakisi katika vigezo vya kweli kutokana na upande mmoja kuwa huru kufanya siasa wakati mwingine ukiendelea kubanwa.
“Sijui hawa Twaweza wametumia vigezo gani katika utafiti wao maana ninachojua mimi vyama vimepigwa marufuku kufanya siasa ila wenzetu CCM pekee ndiyo wanafanya siasa sasa inakuaje mtu anakuja na utafiti wa aina hii,” alisema.
Pia, utafiti huo ulionyesha kuwa idadi ya wanaomuunga mkono Rais John Magufuli imeshuka kutoka asilimia 96 mwaka jana hadi asilimia 71, mwaka huu.
Katika hatua nyingine Chadema imepinga vikali hatua ya Serikali kulifungia gazeti la Mawio kwa muda wa miaka miwili ikisema kitendo hicho ni ishara nyingine ya kuendelea kubinya uhuru wa vyombo vya habari.
Alisema Serikali imechukua uamuzi huo bila kufafanua bayana kifungu kilichokiukwa na zaidi ilizingatia kauli za viongozi waliopiga marafuku kuwajadili marais wastaafu.
Wakati Chadema wakiuponda utafiti wa Twaweza, wabunge wa CCM wao waliusifu hasa katika kipengele cha kuporomoka kwa kukubalika kwa Rais Magufuli, huku wakitaja sababu za kuukubali utafiti huo.
Akizungumza bungeni jana wakati akichangia mjadala wa bajeti, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Lucy Mayenga alisema kilichoelezwa na Twaweza ni sahihi kwa sababu Rais amejielekeza kwa makundi hayo ambayo hayana mtetezi.
“Maskini na watu wa vijijini hao ndiyo watu wengi zaidi. Kiuchumi utafiti huo unakubalika,” alisema Mayenga.
Wakati Mayenga akiendelea kutoa hoja zake, Mbunge wa Mkuranga,(CCM) Abdallah Ulega alitoa taarifa iliyopokelewa na mtoa hoja.
Uledi amesema: “Kwa muda wa utafiti, Rais alikuwa anapambana na vyeti feki, dawa za kulevya na mafisadi. Hao wote hawawezi kumpenda zaidi ya maskini ambao hawaguswi na mambo hayo.”