CCM yampitisha Dk Tulia kugombea uspika

Muktasari:

  • Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, imepitisha jina pekee la Dk Tulia Ackson kuwa mgombea wa kiti cha Spika kilichoachwa wazi na Job Ndugai aliyejiuluzu nafasi hiyo Januari 6, 2022.


Dodoma. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM imepitisha jina pekee la Dk Tulia Ackson kuwa mgombea wa kiti cha Spika kilichoachwa wazi na Job Ndugai aliyejiuluzu nafasi hiyo Januari 6, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Januari 20, 2022 kwenye ukumbi wa White House Dodoma, Katibu Mwenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka amesema Kamati Kuu imepitisha jina moja la Dk Akson kati ya majina 70 ya makada wa CCM waliochukua na kurejesha fomu.

Uratibu wa CCM ni kupeleka majina yasiyozidi matatu kwenye kamati ya wabunge. Wanaweza kupeleka moja au mawili au matatu.

Dk Tulia anakuwa mwanamke wa pili kuwa Spika kama atachaguliwa na wabunge.

Mbali na CCM, chama cha upinzani cha Alliance for Democratic Change (ADC) nacho kimefungua mchakato huo na mwanachama wake, Maimuna Kassim amekuwa wa kwanza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa nafasi ya Spika.

Miongoni mwa wana-CCM walioshindana na Dk Tulia ni wabunge wa sasa, Mussa Azzan Zungu (Ilala), Dk Tulia Ackson (Mbeya Mjini), Luhaga Mpina (Kisesa), Stella Manyanya (Nyasa), Godwin Kunambi (Mlimba) na Joseph Musukuma (Geita Vijijini).

Pia, walikuwamo wabunge wa zamani, Stephen Masele (Shinyanga Mjini), Athuman Mfutakamba (Igalula), Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Profesa Norman Sigalla (Makete), Dk Titus Kamani (Busega), Ezekiel Maige (Masalala) na  Sophia Simba (Viti Maalum).

Kwenye kinyang’anyiro hicho kulikuwa na Bunge wa zamani Thomas Kashilillah, pia walikuwamo watumishi wa umma, makada, viongozi wa zamani wa Serikali na wanafunzi wawili wa vyuo vikuu.

Soma zaidi: Spika Ndugai ajiuzulu