Chadema chataka marekebisho ya mpito ndani ya Katiba ya sasa

Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika akizungumza na viongozi na wananchama wa chama hicho katika ofisi za kanda Victoria baada ya kusimikwa na kupewa jina la Chifu Malonga ikiwa na maana ya kutangaza mambo mema. Picha na Jesse Mikofu

What you need to know:

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania, John Mnyika amesema ili kuwa na tume huru ya uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, yafanyike marekebisho ya mpito kwenye katiba iliyopo sasa.

Mwanza. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania, John Mnyika amesema ili kuwa na Tume huru ya uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, yafanyike marekebisho ya mpito kwenye katiba iliyopo sasa.

Amesema kwa muda uliobaki kabla ya uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba, 2020 haiwezekani kukamilika kwa mchakato mzima wa katiba mpya, lakini inawezekana kufanyika kwa marekebisho ya muda ili kukidhi matakwa ya Watanzania.

Ametoa kauli hiyo leo  Jumapili Desemba 29, 2020 katika ofisi za Chadema Kanda ya Victoria,  baada ya kusimikwa kuwa chifu na wazee wakisukuma na kupewa jina la kichifu la Malonga likiwa na maana ya kutengeneza mambo yawe mazuri.

Mnyika amewaambia viongozi wa kanda hiyo kuwa  hakuna budi  vyama vya upinzani kuungana pamoja na kupeleka muswada bungeni kwa ajili  ya mchakato huo.

“Yapo madai kwamba katiba mpya ni gharama kubwa, lakini Rais John Magufuli akikubali tupeleka muswada wa dharura bungeni tunaweza kufanya marekebisho ya mpito kwenye katiba tuliyonayo bila kusubiria mchakato mzima wa Katiba mpya,” amesema Mnyika.

Amesema Katiba ya sasa inaweza kuongezwa vipengele vitatu ambavyo ni; kuongeza Tume huru ya uchaguzi, ibara inayotaka matokeo ya uchaguzi wa Rais yapingwe mahakamani .

Pia kunaweza kuongezwa  kifungu kinachosema ili mtu atangazwe kuwa mshindi wa urais, lazima awe amezidi asilimia 50 ya kura zote.

Amesema wakati wa uchaguzi mkuu kilikuwapo kipengele cha kupiga kura ya maoni kuhusu aina gani ya katiba inayotakiwa ili wananchi waipigie kura wakati wakichagua wabunge, madiwani na Rais.