Chadema yataja majanga matano yanayowatesa Watanzania

Tabora. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema katika ziara yake ya Operesheni +255 Katiba Mpya iliyofanyika Kanda ya Magharibi kwa siku 11, kimebaini kuwepo kile ilichokiita majanga matano yanayowatesa Watanzania.

Kutokana na uwepo wa majanga hayo, Chadema imetishia kutoshiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025 iwapo mchakato wa kupata Katiba Mpya utakuwa haujakamilika.

Akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika viwanja vya Town School, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alitaja majanga hayo kuwa ni wananchi kushambuliwa wanapoingia hifadhini.

Kutokana na janga hilo, Lissu alipendekeza kuanzishwa utaratibu wa kuvunja mamlaka za uhifadhi zinazokiuka misingi ya haki za binadamu ikiwemo kushambulia raia na kunyang'anya mifugo ya wananchi kwa kinachotajwa kuwa mifugo hiyo imeingia hifadhini.

"Ng'ombe wanakula nyasi kama wanyamapori, tunahitaji aina mpya ya uhifadhi isiyohitaji kutumia bunduki kulinda maisha ya wanyama. Maslahi ya wananchi yanatakiwa kuwekwa mbele, haiwezekani watu wauwawe ili kulinda wanyama," alisema Lissu.

Hata hivyo, Serikali imekuwa ikitoa ufafanuzi wa matukio hayo likiwamo la madai ya Mbunge wa Mbarali aliyotoa bungeni Dodoma Mei 11 kuwa wananchi wa kijiji cha Mwanavala wilayani huko Mkoa wa Mbeya kushambuliwa na askari wa Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Baada ya hoja hiyo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimtuma Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa kutembelea eneo hilo kuona hali ilivyo

Mbali na hilo, alitaja suala la wakimbizi walioishi nchini zaidi ya miaka mitano bila kurejeshwa nchini kwao kunyimwa uraia kinyume na sheria za wakimbizi zinazotaka serikali za nchi zinazowapokea kuwapatia uraia baada ya kuishi miaka mitano katika nchi husika.

"Suala la uraia linahitaji kutatuliwa na Katiba Mpya. Watanzania walioko nje ya nchi waliopata fursa ya kutafuta maisha wananyimwa uraia wakati uraia wao unahitaji kulindwa Katiba Mpya itatatua matatizo yote ya uraia,’’ alisema.

Hata hivyo, Serikali imekuwa ikiwahimiza wakimbizi walioko nchini kurejea katika nchi zao kwa hiari.

Mbali na hayo, Lissu alitaja ufukarishaji wa Watanzania kutokana na tozo, ushuru na vikokotoo na matumizi mabovu ya mali za umma kuwa majanga yanayochangia umaskini kwa wananchi kama ilivyoainishwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2021/22.

"Kama tungezungumza kwa namba, pengine asilimia 60 inachangiwa na kodi, nchi inakamua kila mtu. Serikali haina huruma na mtu yoyote, TRA imekuwa adui wa wafanyabiashara, halmshauri ni adui wa wakulima na wafugaji, ukifuga mifugo ikiwa zizini ni yako ikitoka tu ni yao hii siyo sawa," alisema.

"Tunahitaji kupambana na kulianzisha nchi nzima tumkabili Rais Samia, tumwambie bila Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu hakitaeleweka. Tukikubali kwenda kwenye uchaguzi kama ilivyokuwa mwaka 2019, na tunyamaze kimya milele," aliongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe akihutubia maelfu ya wakazi wa mkoa huo alikosoa baadhi ya viongozi wa Serikali wanaotupa zigo la lawama la ugumu wa maisha kwa hayati John Magufuli pekee kuacha kwani walikuwa sehemu ya mfumo huo.

"Magufuli na Serikali yake, chama chake chote, wabunge na madiwani wake wote walishiriki. Sasa vyama vya upinzani vimenyong'onyea chama pekee kilichobaki kupambana kwa ajili yenu (Watanzania) ni Chadema," alisema Mbowe.

Aliongeza: "Sisi kama Chama tumedhamiria kwamba njia pekee ya kumaliza matatizo haya siyo tu kulalamika lazima tujipange, Watanzania huu msiba wa umaskini mkitegema meza hii (viongozi wa Chadema) peke yake ibadilishe nchi yote mkakaa mkatulia msiba wa umaskini hautakaa uishe," aliongeza

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Catherine Ruge aliwataka watanzania kushirikiana kupigania upatikanaji wa Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi utakaowezesha kupata viongozi ambao ni chaguo la wananchi.

Chadema inaendelea na Operesheni +255 Katiba Mpya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo leo (Jumapili) timu ya Mbowe na Lissu zitafanya mikutano hiyo katika wilaya ya Nzega na Igunga mkoani Tabora huku kikitarajia kuhitimisha mikutano katika kanda hiyo Mei 29, mwaka huu.