Chaja moja kwa simujanja zote yaja

Chaja moja kwa simujanja zote yaja

Muktasari:

  • Umoja wa Ulaya leo umesema kuwa utalazimisha kuwepo kwa chaja (charger) moja itakayoingiliana na simu janja (smartphone) za kampuni zote, uamuzi ambao unaweza kusababisha mzozo na Apple.

Brussels, Ubelgiji (AFP). Umoja wa Ulaya leo umesema kuwa utalazimisha kuwepo kwa chaja (charger) moja itakayoingiliana na simu janja (smartphone) za kampuni zote, uamuzi ambao unaweza kusababisha mzozo na Apple.

Apple inatumia waya zake za kipekee za iPhone.

Kamisheni ya Ulaya inaamini chaja zinazoweza kutumiwa na simu za kampuni tofauti zitapunguza taka za vifaa vya kielektroniki, lakini Apple uamuzi huo utaua ubunifu na kusababisha uchafuzi zaidi wa mazingira.

Umoja wa Ulaya ni soko kubwa lenye watu milioni 450, na kuingiza waya ya USB-C inayoweza kutumika kwa simu tofauti kunaweza kukawa na athari kubwa katika soko la dunia la simu janja.

"Wateja wa Ulaya wamechanganywa kwa muda mrefu wa kutosha na tatizo la chaja kutoingiliana na hivyo kusababisha makabati yao yajae (chaja zisizotumika)," alisema makamu wa rais wa EU, Margrethe Vestager katika taarifa yake.

"Tuliipa sekta hii muda mwingi wa kuja na suluhisho lao, sasa muda umeiva kwa hatua ya bunge kwa ajili ya kuwa na chaja ya aina moja," alisema.

Kwa sasa wateja wanalazimika kuamua kati ya chaja tatu kubwa: Lightning kwa simu za Apple, micro-USB zinazotumiwa na simu za aina nyingi, na USB-C ambazo kuna ongezeko la matumizi yake.

Suala hilo linaanzia mwaka 2009, wakati chaja za aina tofauti zilipokuwa zinatengenezwa kwa ajili ya simu za aina moja na hivyo kusababisha takataka kujaa wakati watumiaji wanaponunua simu za aina nyingine.

EU ilisema hali ya sasa inaendelea kuwa si rafiki na kwamba wateja wa barani Ulaya hutumia takriban dola 2.8 bilioni za Kimarekani (sawa na Sh6.5 bilioni za Kitanzania) kwa mwaka katika simu zenye chaja zisizoingiliana na vifaa vingine vya kielektroniki.

Apple, ambayo inatumia USB-C kwa baadhi ya iPads na kompyuta mpakato zake, inasisitiza kuwa chaja ya aina moja kwa simu zote katika nchi za Umoja wa Ulaya haitakiwi.

"Tunaendelea na msimamo wetu kuwa sheria kali zinazolazimisha chaja ya aina moja kwa simu zote inakandamiza ubunifu badala ya kuhamasisha, kitu ambacho baadaye kitaathiri watumiaji kote duniani," ilisema Apple.