Chamwino Ikulu kuhamishiwa katika jiji la Dodoma

Muktasari:

  •  Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa Dodoma imeridhia pendekezo la Ikulu ya Chamwino kuhamishiwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.


Dodoma. Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa Dodoma imeridhia pendekezo la Ikulu ya Chamwino kuhamishiwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Hayo yamo katika kitabu cha mada zilizowasilishwa leo Alhamisi Machi 17,2022 katika kikao cha RCC.

Uamuzi wa kuridhia mapendekezo hayo ulifanyika katika kikao kilichofanyika Desemba 18, 2021.

“Wajumbe walijadili kwa kwa kina mada hiyo na kutoa hoja mbalimbali. Pamoja na hayo kuridhia eneo la Ikulu ya Chamwino kuhamishiwa katika jiji la Dodoma ikihusisha kata tatu za Msanga, Buigiri na Chamwino” imesema sehemu ya kitabu hicho.

Kikao hicho kiliridhia kwa kuwa kata hizo zitahamia katika Halmashauri ya jiji la Dodoma, Wilaya ya Chamwino iwe na halmashauri mbili ya Mvumi na Chilonwa.

Pia kiliridhia Wilaya ya Dodoma iwe na halmashauri mbili za jiji la Dodoma na Manispaa ya Chamwino.

Aidha, katika kikao hicho cha jana Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema iwapo hawatajadili uchumi wa jamii basi uchumi wa halmashauri utakufa.

“Lazima tujiongeze, ukiniambia future za kwenye halmashauri za Dodoma naweza kuona future kwenye halmashauri za jiji kwasababu miradi yao yote ikitake off hawatategemea kwenye makusanyo,”amesema.

Amesema hategemei baada ya miaka 10 Halmashauri ya Jiji la Dodoma itakwenda kukusanya ushuru wa mazao wagombane na wafanyabiashara wadogo wadogo wanaobeba mabeseni.

Amewataka viongozi wa halmashauri kutumia fursa ya kuanzisha mashamba makubwa ambayo watayamiliki  ili kuongeza mapato ya halmashauri na kwamba Wizara ya Kilimo ipo tayari kuwasaidia kuwezesha hayo kufanikiwa.