Changamoto za mtoto aliyezaliwa bila sehemu ya haja kubwa

Muktasari:
- Afanyiwa upasuaji 16 bila mafanikio, aomba msaada akatibiwe nje ya nchi
Pamoja na kufanyiwa upasuaji mara 16 ili kutafuta njia ya kutolea haja kubwa, changamoto ya mtoto Grace Chaula (12) bado haijapatiwa ufumbuzi.
Hali hiyo inamfanya mama yake kuhaha huku na kule kutafuta msaada wa matibabu nje ya nchi, baada ya matibabu hayo kushindikana hapa nchini.
“Natamani mwanangu Grace apelekwe nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, labda anaweza kupona tatizo alilonalo, kwani ameshafanyiwa upasuaji kama 30 hapa nchini bila mafanikio. Namuomba Rais Samia Suluhu Hassan anisaidie, mimi sina kazi na mume wangu amenikimbia,” anasema Veronica Mwalindu, ambaye anauza machungwa barabarani.
“Baada ya kufanyiwa upasuaji wa kwanza, ilionekana eneo hilo lipo karibu na uke na baada ya upasuaji wa pili ilionekana kuna mfupa ambao ulipelekea kuota majipu na hivyo kuzidisha maumivu kwa binti yangu,” anasema Veronika huku akilia.
“Mwanangu alitolewa utumbo wa haja kubwa nje na kuwekewa colostomy bag ambayo husaidia kinyesi kutoka kwa njia ya utumbo kupitia ukuta wa tumbo.
“Nahitaji msaada kwa sababu kila siku natakiwa ninunue pampasi, huyu binti yangu anavaa pampasi muda wote kwa sababu mkojo unatoka bila taarifa, pia natakiwa kubadilisha mrija kila baada ya siku mbili. Nilikuwa nauza supu lakini kutokana na changamoto ya mwanangu nimejikuta hela yote ya mtaji imekwisha,” anasema.
Anasema kwa kutokuwa na uwezo wa kununua colostomy bag, sasa inambidi atumie vitambaa ambavyo anamuweka ubavuni mwa tumbo kuzuia kinyesi kisidondoke.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mtakatifu Camilius iliyopo Kimara Baruti, Onesmo Mkuwa anasema kutoka na changamoto aliyonayo Veronica, kanisa linamsaidia vifaa vya usafi, pampasi na nauli ya kwenda hospitali.
Daktari anasemaje?
“Grace Chaula ni mgonjwa wangu tangu akiwa mchanga, namjua vizuri sana, yaani ni miongoni mwa watoto waliozaliwa na tatizo la kutokuwa na njia ya haja kubwa,” anasema Daktari bingwa wa upasuaji watoto kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Zaitun Bokhari.
Anasema watoto wengi wanaozaliwa na tatizo hilo hupona baada ya kufanyiwa upasuaji, lakini kwa Grace kumekuwa na changamoto ya kupata njia hiyo kutokana na utumbo wake mkubwa kuwa mfupi.
Ingawa mama wa Grace anasema mwanaye amefanyika upasuaji mara 30, daktari huyo anasema kuwa upasuaji aliofanyiwa hauzidi 16.
“Grace sio tu ana tatizo la kuzaliwa bila kuwa na njia ya haja kubwa, pia ana tatizo katika njia ya mkojo, kwa kitaalamu tunaita neurogenic bladder, ambalo hawezi kuchuchumaa chini na kutoa mkojo kama ilivyo kwa watoto wengine na badala yake anatoa mkojo nje kwa usaidizi wa mpira wa mkojo.
“Hili tatizo limemsumbua sana Grace tangu akiwa mdogo kwa sababu mkojo ukijaa kwenye kibofu unamuuma na aliteseka sana kutokana kupata homa za mara kwa mara na tulikuwa tunamtibu kwa antibiotic. Mara kwa mara amekuwa akilazwa hapa (Muhimbili) kwa ajili ya kumfanyia upasuaji na kusafishwa kibofu cha mkojo na ndio maana utaona amefanyiwa upasuaji nyingi, nyingine ni hizo za njia ya mkojo” anafafanua.
Kwa mujibu wa Dk Bokhari, binti huyo pia amezaliwa na sehemu mbili za siri na kwamba madaktari walishauri atakapofikisha umri kuanzia miaka 12 na kuendelea ndipo watamfanyia upasuaji kubakisha sehemu moja kwa sababu umri huo atakuwa ameshapevuka, hivyo ni rahisi kujua hedhi inatoka sehemu ipi.
Pia anasema mtoto huyo amezaliwa na changamoto ya kuwa na utumbo mfupi, kwani kwa kawaida mtu anatakiwa kuwa na utumbo mkubwa wenye urefu wa sentimita 30, lakini wake una sentimita 15.
“Hali hiyo ndiyo ilisababisha tushindwe kumfanyia upasuaji mkubwa wa kumuwekea njia ya haja kubwa na badala yake tukamfanyia upasuaji wa kumtoboa tumbo kwa pembeni karibu na ubavu wa kulia, ili tutoe utumbo nje na kumuwekewa colostomy bag kwa ajili ya kutolewa kinyesi kwa nje.
“Kutokana na hali hiyo anaweza kutumia colostomy bag katika kipindi chake chote cha maisha kwa ajili ya kutoa kinyesi nje au akipata nchi ambayo wanafanya upasuaji wa kumuwekea utumbo itakuwa ni vizuri zaidi, japokuwa nchi zinazofanya upasuaji wa namna hiyo ni chache,” anaeleza Dk Bokhari.
Daktari huyo anasema tatizo la watoto kuzaliwa bila kuwa na njia ya haja kubwa ni kubwa hapa nchini, kwani kwa wiki huwafanyia upasuaji wa kurekebisha njia ya haja kubwa, watoto nane hadi 10.
“Tatizo hili ni kubwa, kwani kila watoto 10 wanaolazwa, watoto wawili wanazaliwa na tatizo hili ambalo limegawanyika katika makundi mengi,” anasema.
Kundi lingine ni la watoto wanaozaliwa wakiwa na njia ya haja kubwa, lakini sehemu hiyo inakuwa na tundu dogo ambalo humpa shida mtoto anapotaka kutoa choo na kundi lingine ni la watoto wanaotumia tundu katika njia ya mkojo, uzazi na njia ya haja kubwa huungana na kuwa njia moja.
Daktari huyo anasema mtoto mchanga aliyezaliwa na changamoto hiyo hafanyiwi upasuaji kwa sababu hawezi kuvumilia upasuaji mkubwa na wa muda mrefu na sababu nyingine inayozingatiwa na madaktari ni nyama zake bado hazijakomaa na mwili kutoweza kustahimili nguvu ya dawa za usingizi.
Muhimbili yaridhia akatibiwe nje
“Sisi (Hospitali ya Taifa ya Muhimbili) tumeshajiridhisha vya kutosha na tunaweza kusema tumekomea hapo…na kwenda nje ya nchini kwa ajili ya kupata matibabu zaidi ni haki yake kwa sababu huyu ni mtoto mdogo na ana malengo yake, hivyo kama atatokea msamaria mwema wa kumsaidia tupo radhi kabisa, asaidiwe,” anasema Dk Bokhari.
Kuhusu gharama za matibabu, Dk Bokhari anasema kila hospitali iliyopo nje ya nchi ina gharama zake, hivyo ni vigumu kujua gharama na alimuahidi mama Grace atazungumza na moja kati ya madaktari katika hospitali hizo ili wamwambie gharama za matibabu.
Sababu watoto kupata tatizo hilo
Mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Edward Kija anasema hakuna kitu kinachosababisha mtu kuzaa mtoto mwenye tatizo hilo, ila kuna baadhi ya vitu vinavyomuweka mtu katika hatari ya kupata tatizo hilo.
Anasema tatizo hutokana na ajali ya kimaumbile wakati mtoto anapokuwa tumboni ndani ya wiki nane za kwanza. “Hatushauri mama afanye vipimo vya picha (x-ray), MRI, kuwa karibu na mionzi, unywaji holela wa dawa katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito kwa sababu katika kipindi hicho ndio viungo vya binadamu vinatengenezwa,” anasema.
Dk Kija ambaye pia ni daktari bingwa wa watoto kutoka Muhimbili anasema iwapo mjamzito atapata maambukizi ya virusi katika miezi mitatu ya mwanzoni, anaweza kuzaa mtoto mwenye shida katika maumbile ya viungo vya mwili.
Dalili za mtoto mwenye tatizo hilo, ni kukosa choo ndani ya saa 24 za kwanza tangu azaliwe, tumbo kujaa, kutapika, mwili kulegea na kupoteza fahamu.
Anafafanua kuwa wakati wa kunyonya anameza hewa nyingi, pia ndani ya tumbo la mtoto kuna bakteria wanatengeneza gesi na kwamba kwa kuwa hawezi kujamba, ile hewa inabaki tumboni.
Dk Kija anasisitiza wanawake kuwakagua watoto wao ndani ya saa 24 baada ya kujifungua, ili kubaini kama ana tatizo hilo apatiwe matibabu.
Shule yajitolea kumsomesha
Veronica anasema kutokana na changamoto alizonazo alikwenda kuonana na mmiliki wa shule binafsi ya mchepuo wa Kiingereza ya Rosami iliyopo jirani na anapoishi, kuomba mwanaye asome hapo huku akimuelezea changamoto zinazomkabili.
“Mmiliki wa shule hiyo alikubali binti yangu asome bure hadi darasa la tatu na baada ya hapo nilipie, lakini alipofika darasa la tatu aliniambia shule imeona imsomeshe bure hadi darasa la saba. Ada yake kwa mwaka ni Sh 2 milioni ambayo inajumuisha vifaa vya shule, sare na chakula,” anasema.
Mama huyo anasema mwanzoni wanafunzi wenzake na Grace walikuwa hawamuelewi, kwani kuna siku pampasi ilijaa na kusababisha sketi ya shule kulowa, jambo lililomnyima raha na kutaka kuacha kwenda shuleni.
“Grace baada ya kuniambia anachekwa na wenzake shuleni, nilikwenda kuwaeleza walimu na baada ya taarifa hiyo, waliitwa wanafunzi na kuwaonya,” anasema.
Ndoto za kuwa daktari na mchezaji
Akizungumza na Mwananchi, Grace anasema anatamani kusomea udaktari, ili aje kuhudumia watoto wenye shida kama yake.
“Ili nifikie ndoto zangu, namuomba Rais Samia Suluhu Hassan anisaidie, ili nikatibiwe nje ya nchini. Kuna wakati nashindwa kusoma vizuri kwa sababu naumwa tumbo,” anasema. Grace anasema Grace anayesoma darasa la sita.
Pia anasema anapenda kuwa mcheza mpira wa miguu wa kimataifa.