EU yaishika mkono Tanzania matumizi ya nishati safi

Muktasari:
- EU yaunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Mei 8, 2024.
Dar es Salaam. Katika kuunga mkono mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, Umoja wa Ulaya (EU) umetoa magari mawili kwa ajili ya kutoa elimu ya umuhimu wa matumizi ya nishaji hiyo maeneo ya vijijini.
Magari hayo aina ya Toyota Land Cruiser yaliyofungwa mfumo wa sauti kwa ajili ya matangazo kwa umma, yana thamani ya Dola 130,000 za Marekani (Sh340.6 milioni) yametolewa na Shirika la Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) kupitia mradi wa CookFund unaotelezwa nchini.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Mei 8, 2024.
Akizungumza leo Julai 4, 2025 wakati wa hafla ya kukabidhi magari hayo, Balozi wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau amesema kwa sasa matumizi ya nishati safi ya kupikia si anasa, hivyo kila Mtanzanka anapaswa kufikiwa na elimu hiyo.
Amesema EU imeona jitihada zinazofanywa na Tanzania katika kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo lakini bado kuna haja ya hamasa kuwafikia watu wengi zaidi ambao hadi sasa bado wanapika kwa nishati zisizo salama kiafya na zinahatarisha mazingira.
“Tunaona jitihada zinaendelea kufanyika ndiyo maana tumeunga mkono na kusisitiza kwamba, matumizi ya nishati safi si anasa na wala si kwa ajili ya wenye kipato pekee, watu wote wanapaswa kufikiwa na elimu,” amesema.
Amesema kwa hali ya sasa hakuna mbadala wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuwa si tu salama kwa afya za watumiajia bali ni rafiki wa mazingira.

Takribani Watanzania 22,000 wanapoteza maisha kila mwaka nchini kutokana na magonjwa ya upumuaji yanayosababishwa na matumizi ya nishati isiyo salama ya kupikia.
Novemba 1, 2022 katika kongamano la kwanza la kitaifa la nishati safi ya kupikia, Rais Samia alielekeza kuanzishwa kikosi kazi kitakachoshughulikia nishati safi ya kupikia lengo likiwa kuanzisha safari ya kulitoa Taifa kwenye matumizi ya nishati isiyofaa kupikia.
Akizungumza baada ya kupokea magari hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk Khatibu Kazungu amesema Serikali ya Tanzania imejipanga kuhakikisha kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Magari haya yanaenda kutuongezea nguvu katika kufikisha elimu hii kwa umma na utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji na uelimishaji kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo 2034,” amesema.
Katika kufanikisha hilo, Dk Kazungu amewaita wadau wengine kuunga mkono jitihada hizo.
Akizungumzia mpango wa CookFund, mshauri wa masuala ya kitaalamu wa UNCDF, Peter Malika amesema unatekelezwa nchini ukilenga kuchangia katika kutimiza ahadi za Tanzania kuhusu mabadiliko ya tabianchi kwa kuongeza idadi ya watu wanaotumia suluhisho endelevu la nishati safi ya kupikia.
Mpango huo pia unatoa msaada wa kifedha na wa kiufundi kwa kampuni zinazokidhi vigezo ili kuharakisha usambazaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia na kuboresha mazingira.