Chanjo ya kichaa cha mbwa kutolewa bure Arusha, wamiliki waitwa

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Sheria ya Ustawi wa Wanyama Tanzania, ni wajibu wa kila mmiliki wa mbwa kuhakikisha anawadhibiti wasizurure ovyo, wanapatiwa chanjo na kutunzwa kwa usafi na afya njema.
Arusha. Wamiliki wa mbwa mkoani Arusha wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kuwapeleka wanyama wao kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa, katika kampeni maalumu itakayofanyika bure kuanzia Mei 3 hadi 11, mwaka huu.
Kampeni hiyo inaandaliwa na shirika la Mbwa Wa Africa Animal Rescue kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Arusha, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Edgard & Cooper Foundation, kwa lengo la kudhibiti kuenea kwa kichaa cha mbwa miongoni mwa jamii na wanyama wengine.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa Mradi kutoka Mbwa Wa Africa, Jens Fissenebert amesema zaidi ya asilimia 25 ya wananchi Arusha wanamiliki mbwa, huku tafiti zikionesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya mbwa hawajachanjwa, hali inayoongeza uwezekano wa maambukizi kwa binadamu na wanyama.
“Kichaa cha mbwa kinaweza kuzuilika kwa asilimia 100 endapo mbwa wote watachanjwa. Tumelenga kuwafikia watoto wa mbwa, mbwa wakubwa, wa kiume na wa kike bila kujali aina au umri,” amesema Fissenebert.
Wataalamu wa mifugo wanabainisha kuwa kuishi na mbwa ambaye hajachanjwa ni hatari kwa familia kwani anaweza kusambaza kichaa cha mbwa kupitia kung’atwa, hali ambayo huweza kusababisha kifo kwa binadamu endapo chanjo haitatolewa mapema.
Aidha, mbwa hawa pia huongeza visa vya maambukizi ya magonjwa mengine kama TVT na huchangia kutengwa kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ustawi wa Wanyama Tanzania, ni wajibu wa kila mmiliki wa mbwa kuhakikisha anawadhibiti wasizurure ovyo, wanapatiwa chanjo na kutunzwa kwa usafi na afya njema.
Chanjo hiyo itatolewa bila malipo katika maeneo zaidi ya 20 ya jiji la Arusha ikiwemo ofisi za kata mbalimbali na shule za msingi kama vile Lemara, Kijenge, Olasiti, Kimandolu, na Sakina, kati ya saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.
Mbwa Wa Africa imeeleza kuwa chanjo ya mbwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha afya ya jamii kwa kupunguza visa vya kuumwa na mbwa, ajali, magonjwa ya kuambukiza, na hata mauaji ya wanyama hao kutokana na hofu isiyo ya lazima.