Chongolo awaonya wanaozembea kusimamia miradi

Saturday June 12 2021
ccm pic
By Rajabu Athumani

Handeni. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi,(CCM) Daniel Chongolo ametoa onyo kwa viongozi wa chama hicho na Serikali kuacha tabia ya kutotembelea miradi inayoendelea kwenye maeneo yao mpaka wasikie kiongozi wa kitaifa anakwenda kufanya ziara.

Onyo hilo amelitoa leo Ijumaa, Juni 11, 2021 wakati akizungumza na viongozi wa chama hicho na Serikali mkoa wa Tanga kwenye ziara yake mkoani humo ambapo  amesema kuna baadhi ya viongozi hawatembelei miradi hadi wasikie kuna ziara za wakubwa zao.

Amesema Chama Cha Mapinduzi ndicho chenye ilani lakini wapo viongozi hawafiki na kufuatilia na wakiona kuna changamoto ndio wanaanza kutafuta ufumbuzi kwa kuomba msaada wakati angefuatilia mapema angeweza kutatua tatizo.

"Ni lazima sisi viongozi wa chama kwenye ngazi zote tujue kila mradi unaotekelezwa kwaajili ya wananchi tuusimamie na kuufuatilia ili tusaidie kuhakikisha mradi husika unaleta matokeo,tusipofanya hivyo ni makosa kiutendaji', amesema Chongolo.

Chongolo amewataka viongozi hao kushuka hadi ngazi za chini kufuatilia mambo ya kiutendaji kwakuwa chama kinaanzia chini na sio juu hivyo kila mmoja awajibike kwenye nafasi yake.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu Chongolo,Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Henry Shekifu amepongeza ziara hiyo kwakuwa imeleta faraja kwa viongozi wa mikoa na wilaya kujua kwamba utendaji wao kazi unaonekana.

Advertisement

Amesema pia wananchi wanaweza kufikisha kero zao moja kwa moja kwao katika ziara hizo na ndio sababu wanajitokeza kwa wingi.

Advertisement