Chumba mahakama ya kimbari Arusha kugeuzwa kivutio cha utalii

Dk Stergomena Tax akisaini kitabu
Muktasari:
- Serikali imefikia hatua hiyo baada ya Mahakama ya ICTR iliyokuwa imeweka kambi katika moja ya vyumba vya ukumbi wa mikutano ya kimataifa cha Arusha (AICC), tangu mwaka 1994; kumaliza shughuli zake na kukikabidhi chumba hicho mwaka 2015 kwa Wizara ya Mambo ya Nje.
Arusha. Serikali imeamua kukihifadhi chumba kilichokuwa cha Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (UN-ICTR) , kwa ajili ya kumbukumbu ya kihistoria lakini pia kuwa bidhaa ya utalii nchini.
Serikali imefikia hatua hiyo baada ya UN-ICTR iliyokuwa imeweka kambi katika moja ya vyumba katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), tangu mwaka 1994; kumaliza shughuli zake na kukabidhi chumba hicho mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea chumba hicho, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amesema tangu wakabidhiwe, waliamua kukitunza kama kumbukumbu ya vizazi vijavyo na sasa watakiboresha na kukigeuza kuwa bidhaa mpya ya utalii.
“Kwa sasa tunafanya utaratibu wa kukiboresha na kukiimarisha chumba hiki, kuona namna gani tutatunza mifumo ya mabaki ya vitu mbalimbali ambavyo tumekubaliana vitabaki Tanzania, kwa sababu tuna haki ya kuvitunza kama wenyeji, lakini pia vina maana kubwa kwa mchango wa Tanzania,” amesema.
Kwa mujibu wa waziri huyo, mabaki ya kesi zilizosikilizwa na kuamuriwa hapo, yatahifadhiwa salama ili kutunza historia na kuwa sehemu ya utalii na kwamba baada ya maboresho hayo, watu kutoka mataifa mbalimbali watapenda kuja kupatembelea, kupaangalia lakini pia kujifunza mambo mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Ephraim Mafuru amesema kuwa katika kuonyesha umahiri wa historia ya nchi na ushindi wa kisiasa kwenye mambo ya nje yahusuyo kuleta upatanishi Afrika na maeneo ya Maziwa Makuu, ni sababu nyingine ya utunzwaji wa chumba hicho.
“Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Mahakama ya ICTR haikuwa rahisi wala jambo la ajali, bali ilichagizwa na umahiri wa nchi katika diplomasia ya kuleta amani hasa maeneo ya Maziwa Makuu lakini na Afrika kwa ujumla,” amesema.
Amesema kwa Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mahakama hiyo, kuliifanya kuingia katika historia, hivyo kuwa miongoni mwa nchi tatu pekee duniani, kuwahi kuwa na mahakama ya mauaji ya kimbari.
Mahakama zingine ni International Criminal Tribunal for Yugoslavia (ICTY), na Mechanic for International Criminal Tribunal (IMT) ya Ujerumani.
“Wahusika wamekubali kushea na sisi baadhi ya material ili kukiboresha chumba hiki na kukiimarisha kwa ajili ya kudumisha historia yake, hivyo tutaendelea kukihifadhi kama kumbukumbu ili vizazi vijavyo vipate cha kusema juu ya diplomasia ya amani ya nchi yetu.
ICTR ilianzishwa ili kushughulikia watuhumiwa wa matukio ya mauaji ya halaiki huko nchini Rwanda ambapo zaidi ya Watutsi na Wahutu 800,000 waliuawa, ilifanya kazi hiyo kwa kipindi cha miaka 20 na hatimaye kufunga shughuli zake 2015.