Chunya wajivunia matunda ya uhuru
Muktasari:
Halmshauri ya Wilaya ya Chunya wameadhimisha siku ya Uhuru kwa kufanya usafi hospitali ya Wilaya, kujitolea damu na kuwatembelea wafungwa.
Chunya. Wananchi wa halmshauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wameaswa kudumisha uhuru na umoja tulioachiwa na waasisi wa Taifa la Tanzania pamoja na kushiriki shughuli za kijamii ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana.
Haya yameelezwa Decemba 9 2022 na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka katika maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru, ambapo ameowaongoza wananchi kufanya usafi katika hospitali ya wilaya hiyo sambamba na wananchi kuchangia damu.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya kwa miaka 61 ya uhuru kwa halmshauri ya wilaya hiyp, Mayeka amesema kabla ya Uhuru hakukuwa na hospitali ya wilaya hata moja, bali zahanati mbili pekee.
Hata hivyo, amesema kwa sasa kuna hospitali, zahanati zaidi ya 15 na vituo vya afya 20.
Kwenye upande wa elimu, Mayeka amesema kabla ya uhuru hakukuwa na shule ya sekondari hata moja, lakini sasa kuna shule za sekondari 15, kabla ya uhuru kulikuwa na shule za msingi 5 lakini baada ya Uhuru kuna shule za msingi 85, hivyo ambapo amesema kama wilaya imepiga hatua kimaendeleo.
Ameongeza kuwa kwenye sekta ya madini, awali halmshauri Ilikuwa inapata Sh700,000 za ushuru wa uchimbaji wa dhahabu lakini sasa wanapata Sh100 milioni.
Naye Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya, Darison Andrew amesema hospitali hiyo ni miongoni mwa hospitali kongwe nchini serikali, lakini imeendelea kuboresha majengo mbalimbali na kujenga mapya ambapo hivi karibuni wamepokea Sh900 milioni za ukarabati.
"Tunashukuru Serikali kuendelea kutupatia fedha kwa ajili ya kuboresha majengo ya hospitali kwani kutokana na ongezeko la mji wa Chunya tumekuwa tukipokea wagonjwa wengi ukilinganisha na kipindi Cha nyuma, ameeleza mganga mkuu," amesema.