CRDB yakabidhiwa cheti cha utoaji wa huduma ya bima

Arusha. Kamishna wa bima nchini Dk Baghayo Saqware amekabidhi cheti cha utoaji wa huduma ya bima kwa benki ya CRDB ikiwa ni benki ya kwanza hapa nchini kupata cheti hicho kama kampuni tanzu kuanzisha huduma hiyo .
Akikabidhi cheti hicho leo jijini Arusha, Dk Saqware amesema anataka kuona benki hiyo inafanya kazi katika ubunifu wa hali ya juu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ikilinganishwa na Taasisi zingine ambazo zimekuwa zikifanya kazi kwa mazoea.
Aidha amesema kuwa, kitendo cha benki hiyo kukidhi vigezo na kukabithiwa cheti hicho ni mfano wa kuigwa na Taasisi zingine kwani uwepo wa bima hiyo utasaidia sana kutoa huduma za bima kwa wanachama wake na kukuza pato la Taifa.
Amesema hapo awali walikuwa wakitoa huduma hiyo kama mawakala/madalali lakini kwa sasa itakuwa ikitoa huduma hiyo rasmi kama kampuni ya Bima ya CRDB.
Amefafanua kuwa matarajio ni kuona kuwa benki ya CRDB inatoa mchango mkubwa kwenye sekta ya bima kwani hadi sasa sekta ya bima imekuwa ikichangia pato la Taifa kwa asilimia moja ambayo ni ndogo sana na matarajio ni kufikia asilimia tatu.
"Ni matumaini yangu baada ya kuwa kampuni rasmi ya utoaji wa bima ningependa kuona mnahamasisha Watanzania pamoja na kuwapa elimu juu ya matumizi ya Bima kwani mpaka sasa watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya maswala hayo," amesema.
Aidha amesema benki hiyo inatoa huduma zake kimataifa ikiwemo nchi ya Congo, Burundi na Tanzania ni vizuri ubunifu uliotumika katika nchi hizo utumike kukuza sekta hiyo ya bima .
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Dk Majjid Nsekela amesema amefurahishwa sana kupata cheti hicho kama benki ya kwanza hapa nchini.
Nsekela amesema mbali na kuanza kama mawakala wanajivunia kuona wamekuwa kampuni rasmi ya kutoa huduma ya Bima ambapo amesema wao watajiongeza kuhakikisha wanafikia makundi yote maalumu.
Aidha ametaja makampuni ambayo yatanufaika ni pamoja na wasafarishaji,wakulima wafugaji na viwanda ambapo huduma hizo zitakuwa zinatolewa kwa njia ya kidigitali ili kufikia walengwa waliokusudiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa bima ya CRDB, Wilson Mzava amesema wapo tayari kuwahudumia watanzania kuanzia sasa ambapo wateja wao wategemee utofauti mkubwa endapo watapata majanga ya aina yoyote kwani matarajio ya kampuni hiyo ni kulipa kwa haraka zaidi ili waweze kuona tofauti.
Aidha ameongeza Watanzania kuanzia sasa watarajie kuwepo kwa matawi hayo katika benki ya CRDB pamoja na mawakala kwa ajili ya kupata huduma hiyo ambayo inapatikana nchi nzima.