CRDB yakopesha matrekta maonyesho ya Nanenane

Muktasari:

Mikopo hiyo inakusudia kuhakikisha mchango wa kilimo unaongezeka, benki hiyo inatoa mikopo ya matrekta kuwezesha ulimaji wa eneo kubwa zaidi hivyo kuongeza mavuno

Bariadi. Serikali imewahimiza wakulima kuzingatia kilimo cha kisasa kitakachosaidia kukuza kipato chao hivyo kuwatoa kwenye umasikini.

Hamasa hiyo imetolewa na naibu waziri wa kilimo, Hussein Bashe alipotembelea banda la Benki ya CRDB kwenye uzinduzi wa maonyesho ya 29 ya Nanenane yanayofanika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi vilivyopo Bariadi mkoani Simiyu.

Bashe ameipongeza benki hiyo kwa kuwa mstari wa mbele kuwawezesha wakulima na wajasiriamali waliopo kwenye sekta ya kilimo kwa mikopo ya aina mbalimbali inayotoa.
"Kaulimbiu yenu ya kilimo chetu, viwanda vyetu inaonyesha jinsi mlivyojipanga kuboresha sekta hii muhimu ambayo ni kichocheo kikubwa kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda," amesema Bashe.

Kwa kutumia huduma za benki, amesema itasaidia kuboreha uzalishaji na kuongeza tija ya shughuli za wakulima hivyo kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi
Katika maonyesho hayo, Benki ya CRDB kwa kushirikiana na kampuni ya ETC Agro inatoa mikopo ya pembejeo za kilimo yakiwamo matrekta.

Mkurugenzi wa wateja wadogo na wa kati wa CRDB, Boma Raballa amesema wamejipanga vyema kusaidia kujenga uchumi imara kwa kuimarisha sekta ya kilimo kinachotegemewa kwenye mnyororo wa uzalishaji bidhaa za viwandani.

“Kwa ujumla, zaidi ya asilimia 40 ya mikopo yote itolewayo na CRDB nchini inaelekezwa kwenye kilimo. Mwaka 2018/19, zaidi ya Sh650 bilioni zimetolewa,” amesema.

Katika kiasi hicho, Sh150 bilioni amesema zimeelekezwa kwenye kilimo cha mazao ya biashara na malighafi za viwanda, utengenezaji wa pembejeo, usindikaji na usambazaji.

Kwa kushirikiana na wadau wengine, Benki ya CRDB hutoa mafunzo kwa wakulima kupitia warsha na makongamano ili kuwajengea ufahamu juu ya masuala ya fedha, uwekezaji, masoko na mikopo ya kilimo.

Ofisa mauzo wa benki hiyo kanda ya ziwa mashariki, John Joseph amesema kinachotakiwa kwa mkulima kukopa trekta atalolilipia kwa miaka mitatu ni malipo ya awali, uthibitisho wa Serikali za Mitaa na shamba analomiliki.

“Mteja anatakiwa alipie asilimia 35 ya trekta analolitaka na awe na walau ekari 20 za mashamba anayolima,” amesema Joseph.

Licha ya unafuu huo, amesema benki inasafirishia bure trekta la mteja mpaka shambani kwake, wanalifanyia matengenezo bure kwa mwaka mmoja na kumpa warantii wa miaka miwili.