Daktari Kituo cha Afya Nyangoto auawa kikatili

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyang’oto kilichopo Kata ya Nyamongo, Tarime Vijijini, Dk Isack Sima enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Katika hali ya kushangaza daktari Isack Sima ameuawa kwa kukatwakatwa mapanga na watu wasiojulikana Mei 3, 2023 wakati akitoka kutoa huduma usiku katika kituo chake cha kazi, kituo cha afya Nyang’oto kilichopo Kata ya Nyamongo, Tarime Vijijini.

Dar es Salaam. Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyangoto kilichopo Kata ya Nyamongo, Tarime Vijijini, Dk Isack Sima ameuawa kwa kukatwakatwa mapanga na watu wasiojulikana wakati akitoka kituo chake cha kazi usiku akirejea nyumbani.

 Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Michael Mtenjele ambaye amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kumtaka mwandishi kumtafuta baadaye jioni kwa ufafanuzi zaidi.

Dk Sima ambaye inadaiwa aliuawa Mei 3 zilizopita, taarifa zilizosambaa mitandaoni leo Mei 6, 2023 zimeeleza kuwa juzi alishinda kazini akihudumia wagonjwa hadi usiku.

“Ni kawaida yake kujitoa hata muda wa ziada. Wakati anarudi nyumbani, alikutana na watu waliosimamisha pikipiki yake na kumshambulia kwa mapanga. Amekatwa kichwani, mgongoni, mikononi, miguuni yani hata haielezeki. Ameuawa kinyama,” kilieleza chanzo hicho.

Imeelezwa kuwa Dk Isack baada ya kuhitimu shahada ya udaktari Chuo Kikuu cha Mtakatifu Francisko cha Afya na Sayansi Shirikishi (SFUCHAS) na mafunzo kwa vitendo aliajiriwa kituo cha afya Nyangoto kata ya Nyamongo, Tarime vijijini ambako amefanya kazi kwa miaka miwili kama Mganga Mfawidhi.

Taarifa zinazotolewa na wananchi wa eneo hilo wanamzungumzia Dk Sima kama kijana aliyefanya kazi usiku na mchana, “Hata ukimpigia simu usiku atawasha pikipiki kuja kukuhudumia.”

Kufuatia tukio hilo, Wizara ya Afya imesema inafuatilia kwa kina na aitatoa taarifa rasmi.