Damu ilivyofichua mwanamke aliyefia ndani

Muktasari:
- Mwanamke huyo maarufu kwa jina la ‘Mama Queen’ mwenye watoto watatu, alikuwa anaishi bila mume.
Arusha. Katika tukio lililotokea eneo la Moivaro, Arusha mjini, mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Irene Elface, maarufu Mama Queen, mwenye miaka 39, amefariki dunia akihusishwa na madai ya kutoa mimba.
Irene, mama wa watoto watatu ambaye alikuwa akiishi bila mume, amebainika kufariki dunia baada ya damu zilizokuwa zikivuja kutokea chumba kwake na kuwashtua majirani zake leo asubuhi, Septemba 12, 2024.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo akizungumza na Mwananchi amethibitishia kutokea kwa tukio hilo huku akisema mwili wa mama huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Mkoa wa Mount Meru kwa uchunguzi zaidi na hakuna mtu anayeshikiliwa kwa sasa kuhusiana na tukio hilo.
Shuhuda wa tukio hilo, Nancy Wanjira amesema alipoamka asubuhi saa mbili, aliona damu zikivuja kutoka chumbani kwa jirani yake. “Nikaamua kugonga mlango na kuingia ndani, nikamkuta Irene akiwa amelala chini hana nguo na damu zimetapakaa sakafuni. Kando yake, niliona kichanga. Nikajua huenda mimba imetoka maana alikuwa nayo ya miezi saba, na mtoto amekamilika maana sehemu za siri zinaonekana ni mtoto wa kiume,”amesimulia jirani huyo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Elmanyasi, Emmanuel Mollel amesema alipata taarifa ya tukio hilo saa mbili asubuhi na alifika eneo la tukio na kukuta mwili wa Irene ukiwa sakafuni na kichanga kiko pembeni yake huku damu ikiwa imetapakaa chumba kizima.
“Nilipiga simu kituo cha polisi ili waje kuuchukua mwili na kichanga kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” amesema mwenyekiti huyo.
Mmoja wa marafiki wa marehemu, Honoratha Thomas, alieleza kuwa jana jioni walikuwa pamoja kwenye kijiwe chake cha kuuza mihogo na wakaagana vizuri kabla ya asubuhi ya leo kukuta watu wamejaa nyumbani kwa Irene kushuhudia tukio hilo.
Amesema hakujua kama Irene alikuwa na mimba kwa sababu alikuwa na mwili mkubwa na alikuwa akijitanda kanga muda wote.
Pia amesema watoto wa Irene walikuwa kwa bosi wake mwenye hoteli aliyokuwa akifanyia kazi na walipoagana jana usiku, hakuonyesha dalili yoyote.
“Nimeshangaa kusikia habari za kifo chake asubuhi ya leo,” amesema.