DC aagiza kufuatilia chanzo wanafunzi kukosekana shuleni

Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mayeka Mayeka akimkabidhi mwalimu Steven Mwangolombe kishkwambi. Picha na Mary Mwaisenye

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka atoa maagizo kwa ofisa elimu kuhakikisha anafuatilia mwenendo wa wanafunzi kuripoti shule na kuwataka  watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanahamasisha wazazi wa watoto waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wanawapeleka mara moja kwenye shule walizopangiwa.


Chunya. Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka atoa maagizo kwa ofisa elimu kuhakikisha anafuatilia mwenendo wa wanafunzi kuripoti shule na kuwataka  watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanahamasisha wazazi wa watoto waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wanawapeleka mara moja kwenye shule walizopangiwa.

Mayeka ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika hafla fupi ya kuwakabidhi walimu vishikwambi vilivyotolewa na serikali ambapo katika halmashauri ya Wilaya ya Chunya wamepokea vishkwambi 594 ambavyo vimegawiwa kwa walimu wa shule za sekondari na shule za msingi.
Amesema kuna haja ya kufuatilia hilo kwa haraka kutokana na hali iliyopo kwenye shule za sekondari ambapo ametolea mfano kwa baadhi ya shule ambazo ni kuna changamoto hiyo kuwa ni Isangawana ambayo wanafunzi waliotakiwa kuripoti shule 441 lakini waliolipoti shuleni wiki ya Kwanza ni wanafunzi 21.

Shule nyingine ni Makongolosi waliotakiwa kuripoti shule ni wanafunzi 429 ambapo walioripoti ni 34, Makala Sekondari wanafunzi waliotakiwa kuripoti 228 wiki ya kwanza walioripoti ni 28 na Sangambi wanafunzi waliotakiwa kuripoti shule ni 329 lakini walioripoti wiki la kwanza ni wanafunzi 35.
“Watendaji wa kata na vijiji wahakikishe wanawahimiza wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao kwenye shule walizopangiwa watambue kuwa kutompeleka mtoto shule ni kinyume cha sheria,”amesema Mayeka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Chunya, Bosco Mwanginde akizungumzia changamoto hiyo amesema kuna haja ya ofisa elimu sekondari kufuatilia miongozo kwenye shule hizo ili kujua vigezo vilivyowekwa kama ndio chanzo cha wazazi kutotimiza masharti vifanyiwe marekebisho mara moja ili kuwapunguzia wazazi mzigo.


"Tunaweza kusema wanafunzi hawaripoti shule kumbe wazazi wameshindwa kulipa michango iliyowekwa ni lazima tufuatilie miongozo ya kila shule,” amesema Mwanginde.

Aidha Ofisa Elimu Sekondari, Hamis Mapoto akizungumzia hilo amesema atahakikisha anafuatilia changamoto hiyo kwa kila shule ili kuhakikisha kama kuna vitu vinavyowakwamisha wazazi kupeleka watoto shule vinafanyiwa kazi.