DC aliyekimbia vurugu Burundi 2015 asimulia adha ya kuwa mkimbizi

New Content Item (1)
DC aliyekimbia vurugu Burundi 2015 asimulia adha ya kuwa mkimbizi

Muktasari:

  • Mwaka 2015 ulikuwa wa misukosuko katika siasa za Burundi kufuatia uamuzi wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, marehemu Pierre Nkurunzinza kugombea urais kwa kipindi cha tatu.

Mwaka 2015 ulikuwa wa misukosuko katika siasa za Burundi kufuatia uamuzi wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, marehemu Pierre Nkurunzinza kugombea urais kwa kipindi cha tatu.

Uamuzi huo wa Rais Nkurunzinza aliyeingia madarakani mwaka 2005 uliotangazwa katika mkutano mkuu wa chama cha CNDD-FDD, uliwagawa wanachama, ambapo wengi walionekana kupinga.

Kama hiyo haitoshi, mgawanyiko huo uliingia hadi jeshini, Mei 13, 2005 Meja Jenerali Godefroid Niyombare aliyekuwa mkuu wa shirika la ujasusi nchini Burundi, alitangaza kuupindua utawala wa Rais Nkurunzinza kwa kukiuka matakwa ya raia.

Wakati wa tangazo hilo kwa Serikali, Nkurunzinza alikuwa Tanzania akishiriki mkutano wa viongozi wa jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki uliotishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete kuujadili mzozo huo wa Burundi.

Hata hivyo, baadaye ulitatuliwa na Rais Nkurunziza alirejeshwa madarakani baada ya mapinduzi hayo kushindwa. Pia aliendelea na adhima yake ya kugombea urais na alishinda.

Licha ya ushindi huo, mwangwi wa jaribio la mapinduzi hayo uliendelea kurindima hadi ngazi za chini ambako watu waliokuwa wakipinga Rais Nkurunzinza kugombea urais hawakubaki salama, kwa sababu walisakwa na kukamatwa.

Msako huo ulifanywa na Jeshi la Polisi na wafuasi wa CNDD-FDD waliokuwa wakimuunga mkono Rais Nkurunziza.

Watu waliokuwa wakisakwa ni pamoja na maofisa wa Serikali, wanasiasa na wananchi wa kawaida, wengi wao waliokimbia nchi hiyo.

Miongoni mwa watu waliokimbia nchi hiyo ni Johannes (siyo jina lake halisi), aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya katika moja ya wilaya nchini Burundi kwa kipindi cha miaka minane na hata kupewa tuzo ya uongozi bora na heshima kubwa.

Sasa mkimbizi huyo amepata hifadhi jijini Dar es Salaam akijishughulisha na shughuli ndogondogo ili kujipatia kipato.

Mbali ya kuwa DC, Johannes pia ni baba wa familia mwenye mke na watoto watatu, ila hadi sasa hajui familia yake inaendeleaje kutoka kipindi alipokimbia kutoka Burundi kuja Tanzania mwaka 2015, kuomba hifadhi.

Hiyo ilikuwa ni kutokana na hofu ya usalama wa maisha yake kipindi cha uchaguzi mkuu wa 2015, uliosababisha machafuko na maelfu ya Warundi kuikimbia nchi yao.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, mkimbizi huyo anasema kosa lake lilikuwa ni kutumia haki yake ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wake.

“Mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu, nikiwa mkuu wa wilaya nilikuwa mmoja wanachama wa CNDD-FDD, waliotia saini azimio la kumshauri aliyekuwa Rais wakati huo, Pierre Nkurunziza asigombee awamu ya tatu kwa kuamini atakua anavunja Katiba,” anaanza kusimulia. Anasema uamuzi wa Nkurunziza kugombea awamu ya tatu ulizua hali ya sintofahamu nchini humo, huku baadhi ya wanajeshi wakifanya jaribio la kumpindua.

Baadhi ya watu walikuwa wakipinga uamuzi wa Rais huyo kujiongezea muhula wa tatu kinyume cha Katiba ya Burundi.

Hayo ni matukio yaliyosababisha kuvuruga amani na kusababisha machafuko yaliyovuruga utaratibu wa maisha ya kila siku na kusababisha hofu ya msingi juu ya usalama wa nchi na wananchi.

“Kitendo cha kusaini azimio kulisababisha kuchukuliwa kama adui wa serikali iliyokuwa madarakani wakati huo. Nikaanza kuona hatari ya kifo inanikabili, mwisho nikaamua kukimbia nchi nikiiacha familia yangu nyuma,” anasema Johhanes.

Anasema kwa kuwa alikuwa akiishi karibu na mpaka wa Tanzania, aliamua kuvuka mpaka na kukimbilia wilayani Kibondo na kupata hifadhi kwa kiongozi mmoja pale Kibondo (anamtaja jina).

“Baada ya kuishi pale kwa siku kadhaa nikaamua kukimbilia Kigoma na kujisalimisha Idara ya Wakimbizi ambao nao walinipeleka kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu,” anasema.

Anasema hata pale kambini hapakuwa mahala salama kwa upande wake, kwa sababu kulikuwa na wanasiasa waliokimbia Burundi na walikuwa wakitofautiana kimsimamo. “Mkuu wa kambi alishauri niende Kigoma ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR). Baada ya majadiliano wakanipokea na kunipangia hoteli kwa siku tatu, kisha waliniita na kuhoji tena upya, nikawaeleza kila kitu. Baada ya hapo walinipangia hoteli nyingine kwa wiki mbili na baadaye nikahamishiwa Kambi ya mpito iliyopo Kigoma nilipokaa kwa miezi mitatu,” anasema.

Johannes anasema aliamua kuomba kibali cha kuishi Dar es Salaam kama mkimbizi kutoka kwa mamlaka husika na kufanikiwa kupata kibali hicho kwa sababu za msingi za kiusalama.

Mkimbizi huyo anasema tangu mwaka 2015 alipoondoka Burundi hajui familia yake inaendeleaje.

Haya ndiyo madhara ya vita hiyo iliyozalisha wakimbizi lukuki wakiwamo viongozi wa Serikali.