DC Kigoma aunda kamati kuchunguza athari kuungua soko la mitumba

Soko la mitumba Seremala lililopo Manispaa ya Kigoma Ujiji, lililoungua usiku wa kuamkia Februari 10, 2024. Takribani vibanda 148 vimeungua kati ya 700 vilivyokuwepo sokoni hapo.

Muktasari:

  • S: moto na athari zilizojitokeza katika soko la mitumba Seremala lililopo Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma.

Kigoma. Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kali ameunda kamati ya kuchunguza athari walizopata wafanyabiashara mmoja mmoja na kujua chanzo cha moto uliotokea katika soko la mitumba Seremala lililopo Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Jumla ya vibanda 148 kati ya 700 vimeteketea kwa moto usiku wa kuamkia Februari 10, 2024, saa saba usiku, huku chanzo cha moto kikidaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme.

Akizungumza leo, Februari 13, 2024  mkuu wa wilaya hiyo, Salum Kali amesema timu hiyo itaanza kazi mara moja ikiwa ni pamoja na kubaini idadi ya vibanda vilivyoathiriwa na moto huo.

“Timu hii inahusisha watu mbalimbali katika wilaya yetu kwa upande wa Serikali na upande wa wafanyabiashara akiwemo mwenyekiti wa soko na mwakilishi mmoja wa wafanyabiashara atakayependekezwa, lengo ni kufanya kazi kwa karibu na kupata matokeo kwa haraka,” amesema Kali.

Mwenyekiti wa machinga soko hilo, Jumanne Gwama amesema yeye ni miongoni mwa waliochaguliwa kuunda kamati hiyo kwa niaba ya wafanyabiashara na matumaini yake ni kwamba Serikali itafanya jambo kwao baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo.

Amesema anatamani Serikali iwasaidie wafanyabiashara hao kwa kuwajengea vibanda vipya na kuwapa mitaji, ili waweze kuendelea na biashara zao kama awali.

Mfanyabiashara wa bidhaa za jumla na rejareja, Ng’ulu Negaga amesema hatua ya Serikali kuunda kamati na kuchunguza chanzo cha moto pamoja na hasara walizopata wafanyabiashara ni jambo nzuri kama watayafanyia kazi na wao kulipwa fidiwa.

Amesema aliunguliwa na fedha alizokuwa ameacha ndani ya kibanda chake zaidi ya Sh4 milioni ambazo ni mauzo ya takribani siku nne na zilitakiwa kwenda benki siku inayofuata.

Amesema mzigo wake wote uliungua una thamani ya zaidi ya Sh20 milioni kwa sababu anauza vitu mbalimbali kama mabegi, mikanda, viatu vya watoto, mikoba na mikanda kwa jumla na reja reja.

Naye Diana Prosper, amesema kwenye kibanda chake cha biashara kulikuwa na mabelo matatu ya nguo na ambapo kila belo alinunua Sh500,000 na yote yameungua, kwani hakuweza kuokoa hata nguo moja.

“Mimi ni mfanyabiashara wa nguo za kike na ndani mzigo wangu wote umeungua ambao nikipiga hesabu kwa haraka haraka inafika zaidi ya Sh8 milioni nimepoteza, unaweza kuona ni hasara kiasi gani tumepata kama wafanyabiashara wadogo.

“Hizi fedha tulikopa kwenye vikundi kwa ajili ya kuendesha biashara zetu, tulipe kodi ya Serikali na kuendesha familia zetu ikiwemo kusomesha watoto,” amesema Jasmin Shaibu.