DC Kishapu aipa jamii wajibu kupiga vita ukatili

Baadhi ya wazazi wa Wilaya ya Kishapu wakisubiri huduma katika Hospitali ya wilaya hiyo. Picha na Suzy Butondo
Muktasari:
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kiongozi huyo amewasihi wananchi kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuchangia kwa hali na mali utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao huku akiahidi utayari wa Serikali wa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.
Shinyanga. Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude amewaomba wakazi wa wilaya hiyo kushiriki vita dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia kwa kutoa taarifa kwa mamlaka na viongozi katika maeneo yao kuwezesha wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Familia Duniani, Mkude amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wa malezi na makuzi kwa kuzungumza na watoto wao kuhusu vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsi ili kuwawezesha kuvitambua wanapofanyiwa na kutoa taarifa.
‘’Watoto waliolelewa na kukuzwa katika misingi bora, ya haki na usawa wakikua watajenga jamii bora yenye watu wanaoishi kwa kutenda haki kwa wote. Watoto wanaofanyiwa ukatili nao hugeuka kuwa wakatili ukubwani. Kila mzazi na mlezi amlee mtoto wake katika maadili mema,’’ amesema Mkude
Mkuu huyo wa wilaya amehimiza jamii kuachana na mila na desturi potofu ikiwemo Imani za kishirikina, kutweza utu na haki za wanawake na watoto na kuzuia wanawake kumiliki mali.
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kiongozi huyo amewasihi wananchi kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuchangia kwa hali na mali utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao huku akiahidi utayari wa Serikali wa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.
Ametoa maboresho ya miundombinu na huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Kishapu kuwa mingoni mwa jitihada za Serikali za kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
Diwani wa Kata ya Kishapu, Joel Ndettoson amesisitiza umuhimu wa elimu kwa umma kama nyenzo ya kufanikisha vita dhidi ya vitendo vya utatili na unyanyasaji kijinsia.
‘’Tuwafunze watoto wetu maadili mema wangali wadogo huku tukiwakanya kuacha kujiingiza kwenye makundi maovu,’’ amesema Ndettoson
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kishapu, Mwajuma Liyanga ameitaka jamii, hasa wazazi na walezi kuvunja ukimya kwa kukemea na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsi vinavyotokea kuanzia ngazi ya familia, mitaa na jamii kwa ujumla.
‘’Wazazi na walezi wajenge utamaduni wa kutenga muda kuzungumza na watoto wao kufahamu mambo mema na mabaya wanayokutana nayo nyumbani, mitaani na hata shuleni. Kwa kufanya hivyo ndipo tutabaini matatizo ya watoto wetu na kuyashughulikia mapema,’’ amesema Mwajuma