DC Moyo atishia kufunga mgodi kisa uchafuzi wa mazingira

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamedi Moyo aliye vaa kofia akiwa kwenye moja ya maeneo ya mgodi.
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamedi Moyo ametishia kuufunga mgodi wa madini wa Nditi uliopo katika Kata ya Nditi kutokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na wachimbaji hao.
Nachingwea. Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamedi Moyo ametishia kuufunga mgodi wa madini wa Nditi uliopo katika Kata ya Nditi kutokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na wachimbaji hao.
DC Moyo amesema kuwa anatoa onyo kwa wachimbaji hao wadogo kuacha kutiririsha maji machafu kuelekea mtoni pamoja na kuchimba mashimo na kuyatelekeza huku akiwataka waache tabia hiyo.
"Nilikuwa na mpango wakuufunga kwanza mgodi mpaka mtakapofuata maelekezo mliyopewa na ofisi ya mazingira ndipo niufungue ila sitafanya hivyo nimepata ushauri kutoka kwa wazee wakijiji, ofisa madini na mwenyekiti wa umoja wa wachimbaji wadogo.
“Wananchi wengi wananufaika na eneo hili basi ninawapa mwezi mmoja msipotekeleza mlioambiwa na Serikali itakuja kutoa maamuzi mengine,"amesema DC Moyo
Aidha, Moyo amewataka wachimbaji wadogo wazingatie usalama wao kwani wengi hawazingatii alisema unamkuta mtu amevaa pensi hana hata kofia ngumu.
Naye Katibu wa Umoja wa Wachimbaji Wadogo, Castori Joseph amekiri kuwa kuna mahali hawako sawa kwenye swala la mazingira huku akiahidi watayafanyia kazi.
Naye Mtendaji wa Kata ya Nditi, Octavian Gilberth amesema walikagua mazingira hayo na kukuta uchafuzi huo.