Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC Same aagiza uongozi halmashauri kuhamisha gulio

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni akizungumza na wafanyabiashara pamoja na wananchi katika viwanja vya Kwasakwasa, wilayani humo.

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kuhamisha gulio ambalo limekuwa likifanyika kuanzia Jumatano hadi Jumapili kwenye eneo la Kwasakwasa eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya michezo.

Same. Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kuhamisha gulio ambalo limekuwa likifanyika kuanzia Jumatano hadi Jumapili kwenye eneo la Kwasakwasa eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya michezo.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa maagizo hayo leo, wakati alipofanya ziara ya kutembelea  na kukagua soko hilo kuu wilayani Same ambapo pamoja na mambo mengine ametaka miundo mbinu ya eneo hilo ikiwemo vyoo viwe  vimekarabatiwa ifikapo Septemba mwaka huu.

Amesema eneo hilo baada ya kubadilishwa matumizi limekuwa likilalamikiwa na wadau wa michezo na kwamba wameshindwa kuendesha shughuli za michezo katika uwanja huo ambao unatumika kama eneo la gulio.

"Natoa mwezi mmoja kwa uongozi halmashauri kuhakikisha wamehamisha gulio ambalo limekuwa likifanyika kuanzia Jumatano hadi jumapili kwenye eneo hili ambalo lilitengwa rasmi kwa ajili ya shughuli za michezo, kuendelea kuwepo gulio hili hapa linakwamisha shughuli za michezo na kuleta malalamiko mengi kwa wadau wa michezo na wanashindwa michezo," amesema.

Pamoja na mambo mengine, amesema hajaridhishwa na hali ya soko hilo kutokana na uchafu uliokithiri na kwamba vyoo vinavyotumika katika eneo hilo haviridhishi na kwamba vinahatarisha usalama wa wafanyabiashara katika eneo hilo.

"Hali ya soko hilo kwanza ni chafu sana, vyoo vinavyotumika hapa haviridhishi lakini hapa pia kuna mashimo ya vyoo vya zamani ambayo hayatumiki na hayajafunikwa na vinaweza  kuhatarisha usalama wa wafanyabiashara na wanunuzi wanaokuja katika hili soko. Ninaagiza ifikapo Septemba mwaka huu choo kinachotumika hapa kiwe kimekarabatiwa ili kifae kwa matumizi ya binadamu," amesema Dc Kasilda.

"Natoa siku tatu kwa halmashauri mashimo hayo yawe yamefukiwa, uchafu unaozalishwa humo uzolewa kila baada ya siku walizojipangia na wakati wote eneo hili liwe safi  ili kulinda afya za wananchi," amesema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wafanyabaishara pamoja na wananchi wanaotumia soko hilo wamesema kuwa eneo hilo limekuwa siyo rafiki kutokana na ubovu wa miundo mbinu iliyopo katika eneo hilo.

Amani Mshana, mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo, amesema wamekuwa wakifanyabiashara katika mazingira magumu kutokana na ubovu wa miundo mbinu iliyopo katika soko hilo na kwamba wanashindwa kufanyabiashara ilhali halmashauri inachukuwa ushuru.

"Hapa sokoni miundombinu iliyopo siyo rafiki kabisa, ukiangalia vyoo tunavyotumia ni vibovu na vinahatarisha usalama wa afya zetu, tunaomba kama kuna uwezekano wa maboresho yafanyike ili afya zetu ziwe salama," amesema.

Rofina Mdee, mmoja wa wananchi wanaotumia soko hilo, ameiomba Serikali kufanya maboresho katika soko hilo, ambapo amesema ndani ya soko hilo kumekuwepo na mashimo makubwa ambayo yapo wazi jambo ambalo amesema ni hatari hasa wakati wa msimu wa mvua.