DED Siha apiga marufuku michango chakula cha mitihani
Mkurungenzi mtendaji halmshauri Siha mkoani Kilimanjaro Haji Mnasi.
Muktasari:
- Katazo hilo limekuja kufuatia malalamiko ya baadhi ya wazazi wa shule za msingi za Sanya Juu na Sanya Hoyee waliodai kuwa walishachanga chakula cha mchana kwa watoto wao.
Siha. Mkurungenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Siha mkoani Kilimanjaro, Haji Mnasi amepiga marufuku shule za msingi kuchangisha wazazi fedha kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wanaofanya mtihani wa darasa la nne.
Katazo hilo limekuja kufuatia malalamiko ya baadhi ya wazazi wa shule za msingi za Sanya Juu na Sanya Hoyee waliodai kuwa walishachanga chakula cha mchana kwa watoto wao.
Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 13, 2023, Mnasi amesema Serikali inayo bajeti kwa ajili ya chakula cha siku za kufanya mitihani.
“Hizo shule tumewaambia wasitishe zoezo hilo mara moja, serikali ina bajeti yake ya wanafunzi kula,” amesema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, baadhi ya wazazi shule hizo wamedai kuchangishwa Sh10, 000 hadi Sh15, 000 kwa ajili ya chakula siku ya mtihani wa darasa la nne inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
"Sisi tumesha changia fedha, maharage na mahindi kwa ajili wanafunzi wapate chakula shulenj,lakini wametuletea michongo mingine tunaomba Mkuu wa Wilaya kufuatilia," amesema mzazi ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Kwa upande wake Mariamu Judika Mkazi wa majengo Sanya juu, amesema wao hawajakataa kuchangia elimu ila michango imekuwa mingi.
“Sasa unaambiwa utoe Sh10, 000 ili mtoto siku hiyo ale pilau na soda, wakati walimu wa kujitolea wanadai tulipe Sh3,000, inawezekanaje?
"Kweli Sh10, 000 ni nyingi kwa mzazi bora watoe Sh3, 000 kwa ajili ya chakula hicho kitatosha kwa watoto 70," amesema Mariamu
Naye Frank Lazaro Mkazi wa Sanya Hoyee amesema wameshatoa michango yote na kwamba hadaiwi.
“Tunaambiwa tuchangie fedha hizo kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la nne ili watoto siku hiyo wapate pilau na soda shuleni mimi nafikiri kile tulichokitoa kinatosha hatuna uwezo,” amesema.
Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa shule ya msingi Sanya Juu, Ramadhani Mollel, amesema yalikuwa ni makubaliano na wazazi kwenye kikao chao.