Kilimo cha bangi Mara chapungua kwa asilimia 80
Muktasari:
- Hatua hiyo ni matokeo ya operesheni zinazoendelea kufanywa mkoani humo zinazolenga kutokomeza mashamba ya bangi, kukamata wanaojihusisha na uzalishaji na kuvuruga mitandao ya biashara ya dawa hizo.
Dar es Salaam. Mkoa wa Mara ambao kwa muda mrefu ulitajwa miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na uzalishaji mkubwa wa bangi nchini, umeanza kuona mabadiliko makubwa baada ya kilimo hicho kupungua kwa takribani asilimia 80.
Kupungua huko kumeelezwa kuwa ni matokeo ya operesheni zinazoendelea kufanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ambazo zimekuwa zikilenga kutokomeza mashamba ya bangi, kukamata wanaojihusisha na uzalishaji na kuvuruga mitandao ya biashara ya dawa hizo.
Akizungumza leo Julai 24, 2026 Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema kuwa hali ya kilimo cha bangi mkoani Mara imebadilika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita, baada ya Serikali kuimarisha mapambano dhidi ya uzalishaji wa dawa hizo.
Kamishna Janerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo akishiriki kufyeka bangi iliyokutwa katika mojawapo ya mashamba wilayani Tarime.
Amesema kabla ya hatua hizo, baadhi ya maeneo ya mkoa huo yalikuwa yakitajwa kuwa ngome za kilimo cha bangi, huku baadhi ya wakazi wakitegemea zao hilo kama chanzo cha kipato licha ya madhara yake kijamii na kiusalama.
"Mwaka 2024 tuliteketeza zaidi ya ekari 3,500 za mashamba ya bangi katika Mkoa wa Mara. Hatua hiyo imechangia kwa kiwango kikubwa kupunguza uzalishaji wa bangi na kudhoofisha mitandao iliyokuwa ikiendesha shughuli hiyo," amesema Lyimo.
Kauli hiyo ameitoa baada ya kuhitimisha operesheni maalumu zilizofanyika katika Wilaya za Tarime na Rorya, ambapo amesema mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 291.2 yaliteketezwa.
Bangi changa ikiwa imechipua kama ilivyokutwa wakati wa operesheni ya kuteketeza zao hilo haramu wakati wa operesheni iliyofanywa na DCEA mkoani Mara.
Amesema katika operesheni hizo magunia 15 ya bangi kavu yalikamatwa pamoja na pikipiki nne zilizokuwa zikitumika katika shughuli hizo, huku watu wawili wakikamatwa na uchunguzi ukiendelea kuwabaini washirika wengine.
"Matokeo haya yanaonesha kuwa juhudi za Serikali zinaendelea kuzaa matunda. Wananchi wengi wameanza kuachana na kilimo cha bangi na kuelekeza nguvu zao kwenye shughuli halali zinazowanufaisha wao, familia zao na Taifa," amesema.
Kamishna Jenerali huyo amewataka wananchi ambao bado wanajihusisha na kilimo cha bangi kuacha mara moja na kuelekeza nguvu zao kwenye shughuli halali za kiuchumi.
“Niwaombe wananchi washirikiane na DCEA na vyombo vingine vya dola kwa kutoa taarifa za siri kuhusu watu wanaojihusisha na uzalishaji, usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.Kwa upande wetu tutaendelea kuimarisha doria, operesheni na uchunguzi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wanaojihusisha na dawa za kulevya wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria” amesema Lyimo.
Mojawapo ya mashamba ya bangi yakiteketezwa katika operesheni iliyofanyika mkoani Mara.
Akizungumzia hali ilivyo kwa sasa Ofisa Tarafa wa Nchaje, Stephano Peter Kiabaroti, amesema operesheni za mara kwa mara zimesaidia kubadilisha mtazamo wa wananchi waliokuwa wakitegemea kilimo cha bangi.
Amesema uwekezaji unaofanywa na katika kuimarisha taasisi za ulinzi na udhibiti umeongeza uwezo wa kufikia maeneo ambayo awali yalikuwa magumu kufikika.
"Wananchi wengi waliokuwa wakitegemea kilimo hicho sasa wamehamia kwenye kilimo cha mazao ya chakula na biashara pamoja na ufugaji. Hii imeanza kuleta matokeo chanya kwa familia na jamii," amesema.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nkerege, Joseph Mwita Ryoba, amesema kijiji hicho kilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi na kilimo cha bangi kabla ya operesheni za Serikali kuanza kuimarishwa.
Amesema mwaka 2024 pekee zaidi ya ekari 3,000 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika eneo hilo, jambo lililosaidia kupunguza uzalishaji wa zao hilo haramu.
"Kwa sasa wananchi wengi wameachana na kilimo hicho na wameanza kushiriki katika shughuli halali za uzalishaji. Uelewa wa jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya umeongezeka," amesema.
Naye Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Rozana, Kurwa Robert, amesema awali biashara na matumizi ya bangi yalikuwa yakiambatana na changamoto za kiusalama katika maeneo yao.
Amesema baadhi ya vijana walivutwa na biashara hiyo na kuingia katika makundi ya uhalifu, hali iliyosababisha hofu kwa wananchi.
"Baada ya DCEA kuimarisha operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi, hali ya usalama imeimarika. Wananchi wameanza kurejea kwenye shughuli zao za kila siku kwa utulivu," amesema Robert.