Deni la Taifa lapaa, wachumi waeleza

Muktasari:

  • Deni la Taifa Machi 2023 limeongezeka hadi kufikia Sh 94.8 trilioni kutokea Sh87 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 8.9 huku sababu mbalimbali zikitajwa ikiwemo miradi ya kimkakati inayotekelezwa.

Dar es Salaam.  Ripoti ya kila mwenzi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu mwenendo wa uchumi (MER) Aprili, inaonyesha deni la Taifa limeongezeka kwa asilimia 8.9 mwaka 2023 ikilinganishwa na wakati kama huo 2022.

Katika ripoti hiyo inaonyesha hadi mwishoni mwa Machi 2023 jumla ya deni lote (Serikali na sekta binafsi) ni Sh94.8 trilioni ikiongezeka kutokea Sh87 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2022.

Mbali na ongezeko hilo, ripoti hiyo inaonyesha karibia robo tatu ya deni la Taifa ni deni la nje.

“Katika deni lote la Taifa, deni la nje lilikuwa asilimia 71.8,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, deni la ndani la Serikali nalo linazidi kupaa kwa miaka mitatu mfululizo ambapo Machi 2021 lilikuwa Sh16.1 trilioni, Machi 2022 liliongezeka hadi Sh21.7 trilioni kabla ya kupaa zaidi na kufikia Sh26.9 trilioni.

Akizungumzia maana ya kuongezeka kwa deni hilo, Mchumi Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora amesema endapo uwekezaji mzuri unafanyika katika mikopo inayochukuliwa uchumi utaendelea kukua.

“Deni la Taifa linavyozidi kukua ndio uchumi wa nchi unakuwa na nafasi ya kuongezeka kama fedha zinazokopwa zinawekezwa vizuri, kwasababu mtaji wa kufanya miradi mbalimbali unakuwepo,” amesema.

Pia, Profesa Kamuzora amesema mzunguko wa fedha unaongezeka kama fedha zinazokopwa zinaingia katika miradi.

“Kwa nchi ya Tanzania sasa hivi uwekezaji mkubwa unafanyika na ili uchumi uongezeke lazima ukope kwa ajili ya kutimiza miradi hiyo na mzunguko wa fedha uzidi kuongezeka

“Unajua hata nchi zilizoendelea zinakopa kwa ajili ya kufanya miradi mbalimbali na kuongeza mzunguko wa fedha, sioni shida ya deni kuongezeka kama zinatumika kwa tija na haziingii mifukoni kwa watu,” amesema.

Profesa Kamuzora amesema kuongezeka kwa deni hili kunasababishwa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo Serikali inafanya kama treni ya umeme na ujenzi wa bwawa kufua umeme la Julius Nyerere (JNHP).

Kauli ya Profesa Kamuzora inaenda kinyume na maoni ya mchumi Oscar Mkude ambaye amesema kuongezeka kwa deni hilo ni ishara ya nchi kushindwa kutekeleza miradi yake inayoifanya ndani.

“Kuongezeka kwa deni la Taifa kunaonyesha kuwa uwezo wa Serikali kutekeleza miradi yake kunapungua,” amesema.

Mkude alipoulizwa kuhusu Tanzania kukopa mikopo yenye masharti nafuu kama inaweza kuwa ahueni alisema historia inaonyeshga huko nyuma tumewahi kukopa mikopo ya kibiashara (commercial loans) ambayo inatuumiza sasa.

“Deni lenye masharti nafuu ni zuri katika uchumi wa nchi lakini Tanzania katika awamu ya tano nahisi kuna baadhi ya mikopo ilikuwa ni ya kibiashara ambayo ina riba kubwa kutokana na hali ya kidiplomasia ya wakati huo,” amesema.

Akitoa njia ya kulipunguza deni hilo, Mkude amesema ni wakati wanchi kujikita katika kuongeza tija ya mauzo ya nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni ambazo zitasaidia kulipa madeni hayo.

“Lazima tujitahidi kuongeza mauzo ya nje ya nchi ya bidhaa zetu (export) kwasababu madeni mengi yanalipwa na fedha za kigeni ambazo ushuru wetu wa ndani kwa kiasi kikubwa ni fedha za kitanzania,”amesema.

Vigezo nchi kutokopesheka

Profesa Kamuzora amesema ili nchi kufikia vigezo vya kushindwa kukopesheka lazima kuwe na ishara za kushindwa kulipa kile ambacho wamekopa, japo inategemea na aina ya mkopo.

Naye Mkude amesema mbali na kushindwa kulipa madeni lakini pia kama ukuaji wa uchumi wa nchi husika ni mdogo, ni wazi kuwa haiwezi kukopesheka.

“Nichi inashindwa kukopesheka endapo ikishindwa kulipa madeni yake na ukuaji wake wa uchumi ukiwa hasi au mdogo sana,” amesema Mkude.

Aprili 24, 2023 Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Dunia (IMF), Antoinette Sayeh alisema deni la Tanzania ni la wastani na kwamba ni himilivu.

“Deni la Tanzania bado ni la wastani na himilivu, lakini ni muhimu kuendelea kuweka kipaumbele katika mikopo yenye riba nafuu,”

Kauli hiyo aliitoa baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya IMF kuridhia kuikopesha Tanzania dola 153 milioni (Sh358.9 bilioni) kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa bajeti yake ya Serikali.