Dhambi inatoka wapi kutamani cheo cha IGP?

Muktasari:

  • Wale watoto wa Yakobo walichukizwa na kitendo cha mdogo wao Yusuf kuota ndoto zilizoonyesha kuwa siku moja watamuinamia kumsujudu. Kosa la Yusuf lilikuwa ni kuwashirikisha ndugu zake kuhusu maono yake.

Wale watoto wa Yakobo walichukizwa na kitendo cha mdogo wao Yusuf kuota ndoto zilizoonyesha kuwa siku moja watamuinamia kumsujudu. Kosa la Yusuf lilikuwa ni kuwashirikisha ndugu zake kuhusu maono yake.

Alikuwa ameota kuwa siku moja walikuwa shambani wakifunga migabda, ghafla mganda wake ukainuka na ile ya ndugu zake ikauzunguka mganda wake na kuuinamia. Ndugu zake wakatafsiri kuwa siku moja watamsujudu mdogo wao. Chuki zao dhidi yake zikaongezeka.

Na adhabu yake, kwanza ilifikiriwa iwe kumuua lakini ndugu zake wakaogopa damu yake. Wakapata wazo la pili la kumuuza kwa wafanyabiashara wa Misri na wakafanikisha hilo.

Lakini baada ya njaa kuikumba nchi yao, wakalazimika kwenda nchi ya wale wafanyabiashara waliomnunua Yusuf. Kumbe huko Yusuf alikuwa na cheo mithili ya waziri mkuu na ndipo ile ndoto ilipotimia ya kumsujudia mdogo wao.

Kuwa na ndoto si kitu kibaya. Mtu yeyote kwenye kazi yake au kwenye fani yake huwa na ndoto ya kushika nafasi ya juu kabisa katika fani hiyo. Lakini baadhi ya nafasi haziji kwa elimu au jitihada binafsi, bali kuonekana, hasa zile za uteuzi.

Ndivyo Kamanda Wankyo Nyigesa alivyoota kwa sauti kuhusu ufanisi anaofikiria kuuongeza iwapo atateuliwa kushika nafasi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Kamanda Simon Sirro.

Kamanda Nyigesa alikuwa na ndoto kubwa, lakini akashangaa kuona uteuzi unampita kando.

"Nilikuwa najiandaa kuwa DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai), ikachukuliwa," alisema katika hafla ya kumuaga kutoka mkoani Pwani kuhamia Kagera.

"Nikajiandaa kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar, wakachukua. Sasa najiandaa kuwa IGP. Naamini Rais Samia maombi yangu anayasikia. Siku moja tafadhari niteue.

"Mimi naamini nitafanya makubwa. Huwa ninaomba sana mama siku moja aniote tu halafu anitamke tu niwe IGP. Mimi nitamuomba nifanye miaka mitatu halafu nimwambie mama nakukabidhi, naondoka. Unaonaje hapo?"

Ndivyo Kamanda Nyigesa anavyoota iwapo atapata bahati ya 'kuotwa' na Rais Samia, halafu atamkwe kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi. Lakini aliweka bayana kuwa hamu yake ya kushika wadhifa huo haitokani na kuona kamanda wa sasa hatekelezi majukumu yake ipasavyo, bali jinsi anavyojiona anaweza kufanya makubwa zaidi.

Pengine kuna utovu wa nidhamu katika kauli yake, lakini sidhani kama ni kosa kuwaza kushika nafasi hiyo ya juu kabisa katika taasisi hiyo kwa mtu aliyefikia wadhifa wake.

Na hii ni ndoto ambayo maofisa wote wa polisi-- hata ambao hawajafikia cheo cha Nyigesa-- wanayo. Wanaota kuwa siku moja wanaweza kustukia wanateuliwa na Rais kushika nafasi ya IGP. Ingawa hawawezi kuteuliwa wote kwa wakati mmoja kushika wadhifa huo.

Na ndoto hizo zinakuwa kubwa zaidi wakati huu ambao Sirro anaweza kustaafu kwa hiari akiwa na miaka 59. Umri wa kustaafu kwa lazima kwa maofisa wa vyeo vya juu wa Jeshi la Polisi ni miaka 60.

Na iwapo una ndoto kama hiyo na una sifa za kuteuliwa, ni muhimu kujiandaa kuwa utafanya nini iwapo bahati hiyo itakuangukia. Inawezekana wako ambao wanaenda kwa waganga kutaka wafanikishiwe haja zao. Wapo wanaoenda kwenye nyumba za ibada na wapo wanaoweza hata kufanya njama ili IGP aliyepo sasa aonekane anavurunda halafu wateuliwe wao.

Lakini Kamanda Nyigesa amekuwa muwazi. Ameweka ndoto yake bayana na hata kumtaja mteuzi kuwa amkumbuke kwa kuwa ana ndoto ya kufanya makubwa ndani ya muda mfupi. Lakini amegeuzwa kuwa Yusuf yule wa kwenye Biblia. Kwamba anayoyaota ni mabaya, yanalenga kuwashusha wakubwa wake na badala ya kutafuta tafsiri ili ndoto hiyo ifanyiwe kazi kujiandaa kwa yanayokuja.

Jeshi la Polisi limemrudisha makao makuu wakati uchunguzi ukiendelea kuona kama kuna utovu wa nidhamu katika kutamani siku moja ateuliwe kuwa IGP, ingawa hakusema huyu aliyepo sasa aondolewe ndipo yeye ateuliwe.

Wapo wanaoota kuwa rais wa nchi hii na wanasema wazi na wapo waliothubutu hata kuwaambia Watanzania wapewe nchi kwa wiki moja tu wafanye makubwa. Ukitaka kujua wapo watu wengi wa aina hiyo, subiri mchakato wa uchaguzi unapofika, ndipo utakapojua kuwa kumbe wapo wengi wanawazia urais.

Wako huru kuwazia urais kwa kuwa si dhambi.Hata kwa CCM, ambayo ina utamaduni wa kumuachia rais aliyepo madarakani fursa ya kugombea peke yake kipindi cha pili, wapo wanaokuwa wanawaza kupambana naye, lakini wanazuiwa na utamaduni huo.

Si dhambi kuota kufanya vizuri zaidi ya bosi wako au kufanya tofauti na bosi wako wa sasa anavyofanya kwa kuwa ndivyo Mwenyezi Mungu alivyotutofautisha kimwili, kifikra, kiakili na kwa jinsi tunavyofanya kazi. Wote tunaweza kuwa na ufanisi, lakini unaotofautiana.

Inawezekana kuwa Kamanda Sirro amefanya makubwa, lakini kuna maeneo mengi ambayo

pengine hajayagusa na pengine ndiyo ambayo Kamanda Nyigesa anafikiri akiteuliwa atayafanya na Jeshi la Polisi litakaa mguu sawa.

Hayo yametokea katika kipindi ambacho Jeshi la Polisi linatakiwa lianze kujitathmini.Hivi karibuni Kamati Kuu ya CCM ililiagiza serikali kuliangalia upya jeshi hilo kutokana na utendaji wake kulalamikiwa na wananchi, hasa uonevu na kubambikia watu kesi.

Rais Samia amekuwa akisema mara kwa mara katika hotuba yake kuhusu malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi na kulitaka jeshi hilo liache mara moja tabia hiyo.

Na hayo yanatokea wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameunda kamati kuchunguza mauaji ambayo maofisa wa polisi wanatuhumiwa kuhusika, hasa mkoani Mtwara na Tanga. Vyombo vya habari pia vimeripoti mara kadhaa malalamiko ya wananchi dhidi ya ndugu zao ambao wanadai wamepoteza maisha wakiwa mikononi mwa polisi.

Zipo video kadhaa zinazosambaa mitandaoni zikionyesha askari wa jeshi hilo wakichukua mlungula kutoka kwa madereva. Hata vyama vya upinzani vimekuwa vikitaka jeshi hilo lifumuliwe na kuundwa upya ili liwe chombo cha wananchi.

Kwa ujumla kuna matukio mengi ambayo yamefanya jeshi hilo kulalamikiwa na wananchi ambao kimsingi ndio walitakiwa walindwe na chombo hicho cha dola.

Katika mazingira kama hayo, Kamanda Nyigesa lazima awe na mkakati wake wa kufanya ili kukiboresha chombo hicho. Pengine anadhani kushughulikia rushwa pekee, kutasafisha machafu yote yanayolalamikiwa na wananchi, na ndio maana anataka miaka mitatu tu.

Ndio, kijeshi anaweza kuwa amekosa lakini kosa hilo linaweza kuwa linatokana kanuni zilizoundwa kwa mtazamo wa kizamani usioruhusu ndoto ambazo ni bayana kwa kila askari kuwekwa bayana.

Kama Kamanda Sirro anaamini unafiki umetawala Jeshi la Polisi, basi unafiki ndio huo wa kutoweka bayana matamanio. Kueleza bayana kuwa anatamani kuteuliwa si unafiki, bali kusemea pembeni ni unafiki ambao unaweza kuambatana na mbinu ovu za kufikia wadhifa huo.