Diamond aeleza alivyoulizwa na Magufuli kuhusu siri ya baba yake mzazi

Diamond aeleza alivyoulizwa na Magufuli kuhusu siri ya baba yake mzazi

Muktasari:

  • Msanii Diamond Platnumz amesema aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli alimpigia simu lilipoibuka sakata la ukweli kuhusu baba yake mzazi  Januari 15, 2021.

Dar es Salaam. Msanii Diamond Platnumz amesema aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli alimpigia simu lilipoibuka sakata la ukweli kuhusu baba yake mzazi  Januari 15, 2021.

Mkali huyo wa wimbo wa Waah aliomshirikisha mwanamuziki wa DCR Congo, Koffi Olomide ameeleza hayo leo Jumamosi Machi 20, 2021 katika shughuli ya kumuaga Magufuli iliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam.

Januari 15, mama mzazi wa msanii huyo, Sanura Kassim, maarufu mama Dangote, alitoa taarifa ya kutikisa mitandao ya kijamii  kwamba aliyekuwa anafahamika kuwa baba mzazi wa msanii huyo si baba mzazi, bali ni baba mlezi.

Ilikuwa inafahamika na wengi kwamba baba mzazi wa Diamond, ni mzee anayefahamika kwa jina la Abdul Jumaa Issack na ndiyo maana majina halisi ya msanii huyo ni Nasseb Abdul Jumaa.

Lakini, mama huyo alisema baba mzazi wa msanii huyo ni Salum Iddy Nyange ambaye ni marehemu.

Mama Dangote alitoa ufafanuzi huo baada ya awali akizungumza na mtangazaji wa kipindi cha Mashamsham kinachorushwa na redio ya Wasafi, mchambuzi wa masuala ya michezo, Mohamed Nyange au ‘Ricardo Momo’ kueleza kuhusu uhusiano kati yake na Diamond kwamba baba yao ni mmoja na alitambulishwa na baba yake mwaka 1999 wakati huo Diamond akiwa na umri wa miaka 10 .

Mama Diamond alisema Mzee Abdul alimkuta akiwa na ujauzito wa Diamond, alivyomueleza ni mimba yake alikataa.

Akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo baada ya kuulizwa nini atakikumbuka kwa Magufuli, Diamond msanii huyo amesema alikuwa akiwasiliana na kiongozi huyo mara kwa mara hata mambo yasiyohusu shughuli za muziki na hata ulipowekwa ukweli kuhusu baba yake halisi, Magufuli alimpigia simu na kumuuliza kuhusu jambo hilo.

“Kwangu kiongozi huyu alikuwa ni zaidi ya rais, alikuwa akinipigia simu na kuzungumza kama mtu na mtoto wake ukiachilia yale mambo ya kazi hivyo nitamkumbuka sana.”

Diamond aeleza alivyoulizwa na Magufuli kuhusu siri ya baba yake mzazi

“Tazama alivyotekeleza miradi mikubwa ndani ya muda mfupi ikiwemo madaraja na mambo mengine na alipokuwa anasema sisi ni matajiri sio matajiri wa hela  mfukoni lakini ni matajiri wa rasilimali,” amesema Diamond.

Akimzungumzia Rais Samia Suluhu Hassan, msanii huyo amesema anamuamini kwani amefanya kazi kwa muda na Magufuli.

“Mwenyewe nimelelewa na mama peke yake hadi kufika hapa, ninaamini atatufikisha pazuri kikubwa kumuombea mema na kuacha maneno madogo ya kumtia presha ili kuendeleza mema aliyoyacha Magufuli,” amesema.