Diamond sasa amegota au…

Diamond sasa amegota au…

Muktasari:

  • Kutoka tuzo za muziki za Kilimanjaro za mwaka 2010 hadi za Afrima za mwaka 2019, Diamond Platnamuz anaweza kuwa ndio mwanamuziki pekee wa Tanzania kutajwa na kushinda tuzo nyingi ndani na nje ya Tanzania.

Dar es Salaam. Kutoka tuzo za muziki za Kilimanjaro za mwaka 2010 hadi za Afrima za mwaka 2019, Diamond Platnamuz anaweza kuwa ndio mwanamuziki pekee wa Tanzania kutajwa na kushinda tuzo nyingi ndani na nje ya Tanzania.

Katika Tuzo za Muziki za Kilimanjaro, Diamond ameshatwaa tuzo 17, kuanzia na mwaka 2010 wakati wimbo wake wa “Kamwambie” uliposhinda tuzo ya wimbo bora wa mwaka na wimbo bora wa R&B na mwaka 2019 wakati aliposhinda tuzo ya Best Live Act.

Hapo katikati amezunguka katika matamasha tofauti barani Afrika, Ulaya na Amerika kwenda kutwaa tuzo au kusikilizia washindi baada ya kutajwa kuwania tuzo.

Na hapa inaonyesha si tu kushinda na kutajwa kuwania tuzo nyingi, bali pia ameshiriki kuwania tuzo nyingi kulinganisha na wasanii wengine Tanzania na si ajabu kwamba sasa ni mwanamuziki mwenye mafanikio makubwa kuliko wasanii wengine wa nchi hii.

Amepita Channel O Music Video Awards, Whasup Africa Music Video, HiPipo Music Awards, Top Ten Tube Music Awards, The Future Music Awards, MTV Europe Music Awards, MTV Africa Music Awards, Black Entertainment Television (BET), African Music Magazine Awards na People’s Awards.

Kote huko alitwaa au kuishia kutangazwa, kitu ambacho ni ushindi kutokana na jinsi wasanii wengi wanavyoingiza kazi zao katika tuzo hizo ambazo mwishoni humpatia sifa mshiriki hata kama hakushinda.

Mwaka 2020, Diamond alijaribu kupata mafanikio ya juu duniani katika muziki alipoingiza kazi zake katika tamasha kubwa la kutunza wasanii la Grammy Music Awards, ambalo kila msanii duniani angependa hata atajwe kuwania tuzo, achilia mbali kushinda.

Hatua hiyo ilifuatia na maombi kwa umma kutaka wamuombee aingie japo katika orodha ya wanaowania, lakini hakufanikiwa na badala yake wapinzani wake wakuu, WizKid na Burna Boy wakaingia na kutwaa tuzo hizo bora duniani.

Burna Boy, ambaye jina lake halisi ni Damini Ebunoluwa Ogulu, alikuwa mwanamuziki wa kwanza wa Nigeria kushinda tuzo kama msanii binafsi baada ya albamu yake ya “Twice as Tall” kushinda tuzo ya Global Music Album, huku Wizkid akiondoka na tuzo baada ya wimbo alioshirikishwa na Beyonce wa “Brown Skill Girl” kushinda tuzo ya Video Bora wa Muziki.

Mwaka 2021, Diamond Platnamuz amekwaa tena kisiki baada ya jitihada zake za kujaribu kushinda tuzo ya Black Entertainment Television (BET) ya Best International Act kugonga mwamba huku Burna Boy akiibuka kidedea.

Katika orodha ya waliokuwa wanawania tuzo hiyo pia yumo Mnigeria mwingine Wizkid, Aya Nakamura (Ufaransa) Emicida (Brazil, Headie One (Uingereza), Young T& Bugsey (Uingereza na Youssopha (Ufaransa).

Kuanguka kwa Diamond katika tuzo hizo kunaanza kuibua maswali kwamba uwezo wake umegota au taasisi yake, menejimenti na wanaomzunguka, hawana uwezo wa kumtoa hapo alipofikia kwenda ngazi ya juu zaidi?

Tangu achomoze barani Afrika baada ya kufanya marudio ya wimbo wa “Number One” aliomshirikisha Davido, hakukuonekana kizuizi chochote ambacho kingemzuia Diamond kung’ara katika matamasha makubwa ya kutuza wasanii. Na kibao cha “Nana” kilisimika ustadi wake, hasa wa kudansi na video na kuonekana hana mpinzani.

Lakini matamasha makubwa kama ya Grammy, ambayo aliwasilisha kazi mwaka huu, Billboard, ambayo hatujui kama ameshawi kuwasilisha kazi na BET, yanamshinda.

Mwaka huu alikumbana na upinzani mkali wa nje ya tamasha kutoka kwa ‘Jamhuri ya Twitter, ambayo iliandaa pingamizi la kutaka aenguliwe kutokana na kumuunga mkono rais aliyepita wa Tanzania kwa madai kuwa Serikali yake ilikuwa inakiuka haki.

Kampeni ilikuwa kali na takriban watu 15,000 walitia saini pingamizi hilo, ambalo kwa namna moja inaweza kuchukuliwa kuwa halikufanikiwa na kwa namna nyingine lilifanikiwa.

Halikufanikiwa kwa sababu hakuenguliwa na waandaaji na akasafiri kwenda kushiriki kama mmoja wa waliotajwa. Lakini lilifanikiwa kwa sababu inawezekana wapigakura walikubaliana na hoja za wapinzani wake na kuamua kutompa kura, kutokana na jinsi mambo ya haki za binadamu yalivyo nyeti katika ulimwengu wa sasa.

Na pengine mwitikio wake katika hoja hizo unaweza kuwa ulitoa picha halisi ya Diamond ni nani, tofauti na kama angekuwa mtulivu na mnyenyekevu asiyetaka kujibishana na watu wa mitandaoni kwa hoja ambazo ulimwengu unaona ‘kuna tatizo’.

Pamoja na wapinzani kuweza kuwa chanzo cha kuanguka kwa Diamond BET, lakini ushindi wake katika matamasha makubwa unaonekana kuanza kugota na hili linaweza kuwa tatizo la wanaomzunguka.

Hivi sasa si kitu cha ajabu kumuona Diamond mitandaoni, akielezea maendeleo yake, kutangaza utajiri wake, magari, fedha na zawadi za mali,  kujibishana na wapinzani wake, ushabiki wake, kuponda taasisi zinazochapisha habari za mali za watu duniani na mambo mengine tofauti.

Hiki ni kiwango cha chini sana kwa mtu aliyefikia ngazi ya juu katika matamasha makubwa duniani na ambaye ameshajivunia utajiri mkubwa kulinganisha na wasanii wengine Tanzania.

Anawaangalia walio nyuma na kuwaonyesha mafanikio yake, lakini inaaminika kuwa katika riadha, mtu anayeongoza mbio akiangalia kutaka kujua walio nyuma wamefikia wapi, hupoteza hatua moja au kasi yake na akifanya hivyo mara kadhaa, hufikiwa na hata kupitwa na wengine.

Ni wakati sasa wa Diamond na timu yake kutulia na kutathmini safari yao ndefu kuanzia Tandale hadi kutikisa New York.


Imeandikwa na Na Angetile Osiah