Diwani wa Buguruni mbaroni kwa tuhuma za rushwa

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemkamata Diwani wa Kata ya Buguruni, Busoro Pazi (CCM), kwa tuhuma za rushwa na wizi wa mali ya umma, katika kile kinachoelezwa kuwa ni mkakati wa taasisi hiyo kuwasaka viongozi wanaotumia vibaya madaraka yao kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Ilala, Sosthenes Kibwengo alithibitisha kukamatwa kwa diwani huyo Aprili 9, 2025 na baadaye kuachiwa kwa dhamana, huku uchunguzi ukiendelea.
“Ni kweli tulimkamata na kumwachia kwa dhamana, lakini bado tunaendelea na uchunguzi kuhusu tuhuma mbalimbali, ikiwemo rushwa na matumizi mabaya ya mali ya umma. Hatutatoa taarifa za kina kwa sasa kwa sababu tunaendelea na kazi yetu,” alisema Kibwengo.
Pazi anatuhumiwa kushirikiana na watu wengine, ambao bado hawajatajwa, katika vitendo vya rushwa na uporaji wa mali za Halmashauri ya Wilaya ya Ilala.
Tuhuma hizo zimechochewa zaidi na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha akiwa na mabunda ya fedha, huku akidai kuwa ana uwezo wa kununua wajumbe wa CCM katika kura ya maoni.
Katika video hiyo, Pazi pia alinukuliwa akisema, “Kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji,” kauli ambayo imeibua hisia tofauti, huku ikielezwa kuwa ni miongoni mwa masuala yanayochunguzwa na Takukuru katika mahojiano na kiongozi huyo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, sehemu ya tuhuma za wizi zinahusiana na vifaa vya ujenzi kutoka katika majengo ya zamani ya Halmashauri yaliyobomolewa katika eneo la Buguruni, ambako sasa kunatarajiwa kujengwa zahanati ya kisasa.
Kukamatwa kwa Pazi kunakuja wakati jitihada za Takukuru zikionekana kuimarika kuelekea uchaguzi mkuu, kwa kuwabana viongozi wa kisiasa na watendaji wa umma wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.