Dk Jafo afafanua hoja za Muungano zinazosumbua

Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Seleman Jafo, akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kuelekea miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar leo jijini Dodoma

Muktasari:

Ikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika kwa maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanzania, Waziri Jaffo amezungumzia kero zinazoendelea kusumbua muungano huo.

Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makami wa Rais (Muun gano na Mazingira) Dk Selemani Jafo amezitaja kero nne ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi kuwa ni pamoja na uletaji wa sukari kutoka Kiwanda cha Mahonda cha Zanzibar katika soko la Tanzania Bara.

Dk Jafo ameyasema hayo leo Jumanne Machi 26, 2024 wakati akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kuelekea miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Aprili 26,  2024.

Amezitaja hoja hizo ni mgawo wa hisa unaotokana na sarafu ya Afrika Mashariki, mgawanyo wa  faida kutoka Benki Kuu na uletaji wa sukari wa Kiwanda cha Mahonda katika soko la Tanzania bara.

Nyingine usafiri wa vyombo vya moto ambayo inataka mtu anapotoka Zanzibar na gari yake, aweze kutembea muda wote Tanzania Bara.

“Kiujumla ni kwamba tumepata mafanikio makubwa kwa sababu kero zimetatuliwa 22 haya ni mafanikio makubwa sana na hasa. Katika kipindi cha sasa ufanisi umekuwa ni mkubwa sana,”amesema.

Dk Jafo amesema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya pamoja mwaka 2006 hadi sasa, kasi ya utatuzi wa changamoto imeongezeka ambapo hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 25 zilizoibuliwa.

 Amesema changamoto nyingi ambazo zilikuwa hazijapatiwa ufumbuzi zimejadiliwa na pande zote mbili za Muungano na kupatiwa ufumbuzi.

Amesema katika kipindi cha awamu ya sita kinachoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na awamu ya nane inayoongozwa na Dk Hussein Mwinyi, zimetatuliwa kero 15, katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 kati ya hoja 18 zilizokuwepo kwa kipindi hicho.

Kuhusu lini watazilimaliza, Dk Jafo aliwatoa hofu Watanzania kuwa kazi inaendelea vizuri na utashi wa viongozi ni wa hali ya juu.

Amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano,  mafanikio makubwa yamepatikana katika huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji, barabara, umeme, utoshelevu wa chakula pamoja na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Amesema kwa upande wa huduma za elimu, shule za msingi zimeongezeka kutoka shule 3,270 mwaka 1961 hadi shule 20,562 mwaka 2024.

Amesema katika upande wa shule za sekondari,  nazo zimeongezeka kutoka shule 41 mwaka 1961 hadi shule 6,511 mwaka 2024.