Kero 7 za muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi

Muktasari:

  • Serikali imetaja kero saba za Muungano ambazo hazijatatuliwa ikisema inaendelea kuzifanyia kazi katika kuzimaliza.

Dodoma. Serikali imetaja kero saba za muungano ambazo hazijatatuliwa, huku ikiahidi kuwa inaendelea kuzifanyia kazi.

Kauli hiyo imetolea bungeni Dodoma leo Mei 20, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Seleman Jafo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Fuoni, Abbas Ali Hassan aliyetaka kujua jitihada za makusudi zinazochukuwa kumaliza kero zilizosalia.

Waziri Jafo amesema katika kipindi cha miaka sita, kero zilizotatuliwa ni 18, ambapo amezitaja ambazo hazijapatiwa ufumbuzi ni pamoja na mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, faida ya Benki Kuu na usajili wa vyombo vya moto.

“Nyingine ni ongozeko la gharama za umeme kutoka Tanesco kwenda ZECO, malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, kodi ya mapato (Paye) na kodi ya mapato inayozuiliwa (Withholding Tax),” amesema Jafo.

Kwa mujibu wa Waziri kero nyingine ni mapendekezo ya tume ya pamoja ya fedha na changamoto ya uingizaji wa sukari katika soko la Tanzania Bara.

Amesema zipo jitihada za makusudi zinazofanyika ili hoja zilizosalia zipate ufumbuzi na kuendelea kuimarisha uratibu wa utatuzi wake.