Watanzania wengi hawana uelewa wa Muungano

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango

Muktasari:

  • Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema kupitia mijadala inayohu Muungano wa Tanzania inaonyesha wananchi wengi hawana uelewa mpana kuhusu Muungano huo.

Dodoma. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema kupitia mijadala inayohu Muungano wa Tanzania inaonyesha wananchi wengi hawana uelewa mpana kuhusu Muungano huo.

 Dk Mpango ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 26, 2022 wakati wa sherehe za miaka 58 ya Muungano wa Tanzania zilizofanyika jijini Dodoma.

Amesema wananchi wengi wamezaliwa baada ya Muungano, hivyo wengi hasa vijana wanaufahamu Muungano ama kwa kusimuliwa au kwa kusoma machapisho mbalimbali.

Dk Mpango amesema kuwa kumekuwepo kwa mijadala mingi kuhusu historia, mantinki aina ya muungano wa nchi mbili (Tanganyika na Zanzibar), faida na changamoto zake.

Amesema kupitia mijadala hiyo inaonyesha kuwa wananchi wengi hawana uelewa mpana kuhusu Muungano.

Dk Mpango amesema hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kuhusu muungano huo na kwamba Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuendelea kuelimisha zaidi juu ya muungano.

Amesema kitabu kinachoitwa Muungano wa Tanzania na Zanzibar, chimbuko, Misingi na Maendeleo ambacho kimezinduliwa leo kimeeleza historia na misingi iliyozesha muungano Tanganyika na Zanzibar kufanyika.

Pia kimeeleza kuimarika na kudumu kwa miaka 58 sasa na jinsi viongozi waaasisi walivyokuwa viongozi wa mfano, waliotanguliza maslahi ya Taifa mbele kabla ya maslahi yao binafsi.

Aidha, amesema kitabu hicho kimeelezea mafanikio mbalimbali, hoja za muungano zilizojitokeza na hatua zilizochukuliwa kuzipatia ufumbuzi. “Kitabu hiki kimeelezea kwa kina utaratibu ambao Serikali mbili zimejiwekea kwa ajili ya kujadili hoja za muungano zinazojitokeza kwa lengo la kuzipatia majawabu ya kudumu,”amesema.

Ameagiza ofisi yake kuhakikisha kuwa kitabu hicho kinapatikana Tanzania Bara na Zanzibar.