Kero 18 za muungano zatatuliwa

Muktasari:

  •  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo amesema wamefanikiwa kutatua kero 18 za muungano kati ya 25 zilizopo.


Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo amesema wamefanikiwa kutatua kero 18 za muungano kati ya 25 zilizopo.

Jafo ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 26, 2022 wakati wa sherehe za miaka 58 ya muungano wa Tanzania na Zanzibar.

Amesema mwaka 2020 waliweza kutatua kero saba na kubaki kero 18 za muungano.

 “Lakini kwa uongozi wenu wewe (Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango) na mheshimiwa Rais (Rais Samia Suluhu Hassan) tumefanikiwa kutatua kero 11 (mwaka 2021) na hivyo ukijumlisha na zile saba zinakuwa 18,”amesema.

Amesema katika sherehe hizo Dk Mpango atazindua kitabu ambacho kinazungumza misingi ya muungano na maendeleo yake na kwamba kitabu hicho ni kitabu pekee tangu muungano ulipoanzishwa.

“Maelekezo yenu yamefanikisha hili, kitabu hichi kitakuwa ni nyenzo kwa Watanzania, nyenzo kwa wadau mbalimbali ya msingi, historia na maendeleo ya muungano katika miaka mbalimbali,”amesema.

Amesema kama itampendeza kinaweza kutumika katika somo la historia shuleni ili kupandikiza agenda ya ufahamu kuhusu muungano wa Tanzania na Zanzibar.