Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Jafo aitaka UNDP kuongeza msaada utunzaji mazingira

Muktasari:

  • Serikali imeipongeza UNDP kwa kuyasaidia mashirika mbalimbali nchini na imeitaka kuendeleza kutoa msaada huo ili taasisi kutekeleza vema programu za utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya Taifa.

Arusha. Serikali imelisihi Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kuendelea kuziwezesha taasisi za mazingira ili zitekelezwe vema programu zao kupitia miradi midogo midogo ya shirika hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Seleman Jafo juzi Februari 11, 2023 Jijini hapa wakati akizindua kitabu cha Maarifa ya Asili na Utunzaji wa Mazingira, kilichoandaliwa na Shirika la Wanahabari la Usaidizi wa Jamii za Pembezoni (Maipac).

Maipac imeandaa kitabu hicho kwa usaidizi wa Shirika la Elimu ya Uraia na Msaada wa Kisheria (CILAO), Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF) Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na halmashauri za wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro za mkoani hapa.

Maarifa ya asili ni maarifa yaliyopo katika jamii ambayo hurithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine kupitia simulizi za mababu, mabibi na wazee mbalimbali katika jamii.

“Niwaombe endeleni kuhakikisha taasisi hizi zinapata uwezeshaji mkubwa ili ziweze kufanya kazi vizuri hasa katika suala la zima la utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya nchi yetu. Lazima tulinde mazingira yetu kwa pamoja,”amesema Dk Jafo.

Kuhusu kitabu hicho, Dk Jafo wizara yake inaapongeza juhudi hizo, akisema zamani mtu akiambiwa msitu una nyoka mkubwa hawezi kwenda.

Amesema hatua hiyo ilisaidia mazingira ya zamani kutunzwa kwa ufanisi, lakini hivi sasa hali imebadilika kutokana na mabadiliko tabianchi.

“Wengi hawana habari hizi za kuhusu elimu ya asili ilivyosaidia binadamu kuishi, lakini sasa masuala haya yamewekwa katika nakala ngumu na laini na wenzetu wa Maipac, nawapongeza maana Taifa letu litapata maarifa mengine ya utunzaji wa mazingira,” amesema Dk Jafo.

Dk Jafo amesema wazee wa zamani walisaidia katika utunzaji wa mazingira kwa kutumia maarifa ya asili, lakini ana furahi kuona Maipac kuchukua mbinu hizo na kuziweka katika kitabu ili kila mtu apata fursa ya kusoma kuhusu utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya Taifa.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Maipac, Mussa Juma amesema kitabu hicho kimebainisha maarifa ya asili yanayotumika katika masuala uhifadhi wa mazingira, utunzaji wa vyanzo vya maji, uhifadhi wa misitu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi miongoni mwa jamii za kimasai zinazoishi Kaskazini mwa Tanzania.

“Katika Kata za Selela na Engaruka zinazopatikana na Wilaya Monduli wenyeji Wamasai hutumia maarifa yao ya asili katika kutunza mazingira na vyanzo vya maji.

“Muda mrefu jamii ya wamasai imekuwa ikiendeleza utamaduni wao wa mila na desturi katika maisha ya kila siku kwa kurithishana kutoka kizazi kimoja hadi kingine hasa wazee Laigwanan wanaofundisha vijana kuhusu mila na desturi hasa katika kutunza mazingira,” amesema Juma.

Kwa upande wake Mratibu wa Miradi Midogo wa UNDP, kupitia GEF, Faustine Ninga ameipongeza Maipac kwa kukamilisha mchakato wa uchapaji wa vitabu hivyo na kuandaa video vya Makala fupi kuhusu maarifa ya asili katika utunzaji wa mazingira.

Naye Katibu wa Baraza la Mila la Kimasai Tanzania, Amani Lukumay amesema kitabu hicho ni cha aina yake kwa sababu kinaelelezea umuhimu wa maarifa ya asili katika uhifadhi wa mazingira na kitakuwa ni urithi muhimu kwa vizazi vijavyo.